Ads

Usafi ni jukumu la kila mwananchi

Na Raymond Mushumbusi 
mwambawahabariblog

Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imesema jukumu la kuzoa maji taka katika maeneo mbalimbali Mjini Kibaha ni la kila mwananchi  na sio kuiachia Halmashauri kazi ya kuwazolea maji taka katika maeneo yao.

Akijibu malalamiko ya wafanyabiashara toka Mjini hapa  kuhusu ukosefu wa gari la kunyonya maji taka katika Halmashauri hiyo, Afisa Habari wa Halmashauri Innocent Byarugaba amesema ni kweli Halmashauri halina gari rasmi la kunyonya maji taka ila wanashirikiana na makampuni binafsi kufanya kazi hiyo.

“Tumeyapata malalamiko hayo toka kwa wafanyabiashara ila nachotaka kuwaambia ni kwamba jukumu la kunyonya maji taka katika maeneo yao ni lao na sio la Halmashauri peke yake hivyo wasilete kisingizio cha Halmashauri kutokuwa na gari la kunyonya maji taka kufungulia maji taka mitaani na katika vyanzo vya maji, huko ni kukiuka sheria na kuendekeza uchafu na tutawachukulia hatua wote watakaobainika”

“ Nawashangaa wafanyabiashara wanaoshindwa kuweka mazingira yao safi kwa kisingizio cha Halmashauri kukosa gari, wakati wao ndio wahusika  na hata wakati wa kupambana  na magonjwa ya mlipuko wao ndio wanaoathirika zaidi, ” alisema Byarugaba.

Byarugaba amesema Halmashauri zinakaribisha makampuni binafsi kuja kuwekeza katika shughuli za unyonyaji  maji taka katika Mji wa Kibaha ili kupunguza athali iliyopo ya utiririshaji maji taka ambao ni hatari kwa afya za wakazi.

Ameongeza kuwa kwa sasa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wanatumia mabwawa ya Shirika la Elimu Kibaha kumwaga maji taka, kutokana na ongezeko la watu Mjini hapo mabwawa hayo hayatoshi tena kwani yalijengwa miaka ya 1960 ambapo wakazi waliokuwa wanatumia walikuwa wachache ukilinganisha na sasa.

Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha katika kutatua tatizo hili ilikaa kikao cha Kamati ya kuboresha usafi wa Mazingira chini ya Mwenyekiti  Innocent Byarugaba  mwezi June mwaka jana ili kujadili ni kwa jinsi gani wataweza kupata gari la kunyonya maji taka litakalosaidia kupunguza tatizo hilo na kuja na maazimio ya kutengea bajeti ya kununua gari hilo.

No comments