Wauzaji bidhaa holela soko la Buguruni wapigwa marufuku
Na Jacquiline Mrisho
mwamawahabariblog
Halmashauri ya Manispaa
ya Ilala yapiga marufuku uuzwaji holela wa bidhaa katika soko la Buguruni
unaochafua mazingira ya soko na kuhatarisha afya za walaji.
Hayo yamesemwa leo na
Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala David Langa wakati akifafanua
kuhusu kero ya wauzaji holela wanaopanga bidhaa chini katika soko la Buguruni.
“Bidhaa zinazopangwa chini katika soko la
Buguruni sio rasmi na hakuna utaratibu unaoruhusu wauzaji kufanya biashara
hiyo, hivyo natoa tahadhari kwa wale wote wenye tabia hiyo kuwa ni marufuku
kufanya biashara ya kupanga bidhaa chini na sio kwa soko la Buguruni tu ila
katika masoko yote yaliyopo katika manispaa yetu” Alisema Langa
Afisa langa amesema kuwa
wapo maaskari wanaolinda na kuthibiti uuzwaji holela wa bidhaa katika soko hilo
ila wauzaji wamekuwa wakifanya mchezo wa kuwavizia maaskari pindi wanapoondoka
ndipo wanapanga bidhaa zao.
Ameongeza kuwa suala
hili limekuwa sugu katika masoko mengi na njia ya kukabiliana na changamoto hii
ni kuongeza askari wengi watakaokaa muda wote ili waweze kukabiliana na wauzaji
holela.
Aidha Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na Maafisa Afya inafatilia kwa karibu masoko
yote ili kufatilia kama wauzaji wanazingatia kanuni za afya kwa kuweka
mazingira safi ili kuokoa afya za walaji.
Uchafu wa mazingira
katika masoko ya Jiji la Dar es Salaam umekithiri na imekuwa ni tatizo sugu
lakini Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imejipanga kupambana nalo ili kuondoa
uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Mwisho
Post a Comment