January Makamba Awafuta Kazi Vigogo Watatu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira-NEMC
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA
MAJUKUMU YA BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA
MAZINGIRA-NEMC
Katika kikao kilichoitishwa na Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tarehe 24 January 2016, kuhusu
kuimarisha utendaji ndani ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira-NEMC maamuzi yaliyofikiwa ni kama ifuatavyo:
1. Kuhusu suala la kiwanda cha kusindika minofu ya punda mkoani Dodoma,
imegundulika kulikuwa na ukiukwaji mkubwa, wa makusudi na wa wazi wa miiko
ya kazi kwa watumishi wa NEMC walioshughulika na kiwanda hicho. Hivyo, Mhe.
Makamba ameagiza watumishi wa NEMC wafuatao wasimamishwe kazi
mara moja:
a. Dkt. Eladius Makene -Afisa Mazingira Mwandamizi,
b. Wakili Heche Suguta Manchare - Mwanasheria Daraja la II
c. Mhandisi Boniface Benedict Kyaruzi, Afisa Mazingira.Hatua nyingine za
kinidhamu na kisheria zitafuatia
2. Vilevile, imebainika kwamba usimamizi wa watumishi wa NEMC siyo makini na thabiti na kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza.
Hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Bonaventura Baya apewe
barua ya onyo kali na la mwisho kwa udhaifu katika usimamizi wa watumishi wa
Baraza.
3. NEMC kama chombo muhimu nchini kilichopewa jukumu la kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira inatarajiwa kazi
zake
zifanyike kwa ufanisi wa kiwango cha juu kulingana na majukumu yaliyoko
kwenye Sheria.
Hivyo, kwa mapungufu yanayojitokeza Mhe. Makamba, ndani ya wiki moja
ataunda jopo la wataalamu wasiozidi watano ili kutathmini utendaji wa NEMC na
changamoto mbali mbali katika usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kuishauri
Serikali ipasavyo.
4. Ili kuimarisha ufanisi na udhibiti wa utendaji wa NEMC, ndani ya wiki moja
litatolewa Tangazo litakalokuwa na mambo yafuatayo:
Anwani ya barua pepe (email), Nukushi (fax), Namba ya simu, Namba ya
Whatsapp ili mtu yeyote mwenye malalamiko au aliyewahi kuombwa rushwa
chochote na watumishi wa NEMC ambacho ni kinyume na maadili ya kazi yao
atoe taarifa mara moja ili uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe.
5. Kutokana na mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa Tathmini ya
Athari kwa Mazingira, ndani ya wiki moja, NEMC ipitie upya orodha ya wataalamu
na taasisi elekezi zilizosajiliwa na kufuta wataalamu na taasisi zote ambazo
zimekuwa zikikiuka maadili ya kazi zao likiwemo suala la kuwasilisha taarifa
zilizo
chini ya viwango, kuchelewesha kazi za wateja wao na kutowasiliana na wateja
wao kuhusu hatua za utekelezaji wa maombi yao.
6. Ndani ya wiki tatu uitishwe mkutano wa dharura wa Bodi ya NEMC kujadili na
kufanya maamuzi juu ya changamoto za utendaji katika Baraza.
IMETOLEWA NA
IDARA YA MAZINGIRA,
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
TAREHE 24.01.2016
Post a Comment