HOTUBA YA KAIMU KATIBU MTENDAJI WA BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI, BI ANNA DOMINICK KATIKA SHEREHE YA KUTOA MIKOPO KUTOKA BENKI YA POSTA KWA VIKUNDI VYA VIKOBA ILIYOFANYIKA DAR ES SALAAM TAREHE 23 DESEMBA 2015
Kaimu Katibu
Mtendaji Wa Baraza La Taifa La Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bi Anna Dominick
Akitoa Hotuba Mbele Ya Wana Vikundi Wa Vicoba Kulia Ni Mkurugenzi Mkuu Wa Bank
Ya Posta Bw Sabasaba Moshingi (Picha na John Luhende)
Ndugu Sabasaba Moshingi, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta,
Ndugu wafanyakazi wa Benki ya Posta,
Ndugu wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,
Ndugu Mkurugenzi wa TAYEEO Taasisi mwamvuli wa VICOBA,
Ndugu Wawakilkishi wa vikundi vya VICOBA,
Ndugu wanahabari,
Mabibi na Mabwana,
Kwanza kabisa ninapenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wote na kuwashukuru kwa kukubali mwaliko wetu kuja kushiriki nasi katika tukio hili muhimu la utoaji wa mikopo kupitia Benki ya Posta chini ya makubaliano maalumu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 14 Julai 2015 tulikutana katika ukumbi huu huu wa Wizara ya Fedha kushuhudia utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Benki ya Posta kudhamini mikopo kwa wajasiriamali kupitia SACCOS na vikundi vya VICOBA.Utekelezaji wake ndiyo unaanza rasmi na niwapongeze kwa kuwa makundi ya awali kuanza kufaidika na mikopo hii. Nafahamu kwamba wote hapa mna majukumu mengine muhimu ambayo mlitakiwa kuyafanya kwa wakati huu lakini pamoja na hayo mmeweza kuyaacha na kuja kushiriki nasi hapa. Tunawashukuru sana.
Pia napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Benki ya Posta kwa kukubali kushirikiana nasi katika kuandaa na kutekeleza makubaliano ya kuwasaidia Watanzania wajasiriamali kupata mikopo ya kutekeleza shughuli zao za kiuchumi kwa masharti nafuu. Vilevile nachukua nafasi hii kuwashukuru watumishi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji na wale wa Benki ya Posta kwa maandalizi mazuri kuhakikisha kuwa shughuli hii inafanikiwa.
Ndugu Washiriki
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa ukosefu wa ajira katika nchi yetu ni moja ya changamoto kubwa zinazowakabili Watanzania na hasa vijana. Hali hii inathibitishwa na matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika hapa nchini. Kwa mfano utafiti wa hali ya nguvu kazi uliofanyika mwaka 2005/2006 unaonyesha kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira kwa nguvukazi yote kwa ujumla ni asilimia 11.7 ikilinganishwa na ukosefu wa ajira wa asilimia 13.4% kwa vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 34. Aidha, kwa mujibu wa takwimu za Ofisi Kuu ya Takwimu ya Taifa ya mwaka 2011 inakadiriwa kuwa vijana wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka ni kati ya 800,000 hadi 1,000,000 ambao wanapigania nafasi za ajira zisizozidi 60,000 katika sekta ya umma na nafasi takribani 300,000 katika sekta binafsi. Hii inamaanisha kuwa kiasi cha vijana kati ya 400,000 hadi 600,000 wanakuwa hawana ajira yoyote kila mwaka hapa nchini.
Ndugu Washiriki
Makubaliano tuliyosaini kati ya Benki ya Posta na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni moja ya michango muhimu katika kukabiliana na tatizo hili kubwa la ajira nchini. Sheria ya Uwezeshaji namba 16 ya mwaka 2004, katika sehemu ya 16, inaelekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mfuko huu ulishaanzishwa tangu mwaka 2008 na pamoja na majukumu mengine unatumika kutoa au kudhamini mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali nchini.
Leo tunashuhudia utekelezaji wa makubaliano yetu na Benki ambapo vikundi nane vya vikoba vitapatiwa mikopo yenye masharti nafuu kwa makubaliano maalumu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mikopo hiyo yenye jumla ya TZS 244,500,000 (Millioni Mia Mbili Arobaini na Nne Mia Tano Elfu tu), itawanufaisha wajasiriamali wanavicoba 185 ambapo kati yao wanawake ni 137 (74%) na wanaume ni 48 (26%). Vikundi vitakavyopata mikopo leo ni ni pamoja na;
Sn
|
Jina la Kikundi
|
Idadi ya Wanachama
|
Kiasi cha mkopo
| |
Wanawake
|
Wanaume
| |||
1
|
Juhudi
|
21
|
9
|
15,500,000
|
2
|
TAYEEO VIKOBA
|
12
|
3
|
30,900,000
|
3
|
Mwanga
|
24
|
1
|
18,800,000
|
4
|
Maendeleo
|
9
|
7
|
28,500,000
|
5
|
Mazingira
|
17
|
13
|
47,000,000
|
6
|
Umoja ni Nguvu
|
7
|
13
|
35,150,000
|
7
|
Gosofu
|
19
|
0
|
18,500,000
|
8
|
Nyota njema
|
28
|
2
|
30,150,000
|
Total
|
137
|
48
|
224,500,000
|
Ndugu Washiriki
Asilimia 74 ya mikopo yote itakayotolewa leo itaelekezwa kwa wanawake ambao ndiyo nguzo ya familia. Baraza linaamini kuwa ukimwezesha mwanamke utakuwa umeiwezesha jamii nzima kwani wanawake ndiyo wanaobeba majukumu mazito katika familia ya utunzaji wa familia na jamii kwa ujumla. Mikopo hii inayotolewa leo itakuwa na riba ya asilimia 11 kwa mwaka.
Ndugu Washiriki
Ningependa kuwaasa wajasiriamali wote watakao pata mikopo hii leo kufanyakazi kwa bidii kama ulivyo msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli ya “Hapa kazi tu”. Aidha napenda kuwahimiza wakopaji kuilekeza mikopo hii katika shughuli za kiuchumi ili waweze kukuza kipato chao na kipato cha taifa kwa ujumla. Pia mnahimizwa kuirejesha mikopo hii kwa wakati ili watanzania wengine nao waweze kunufaika.
Ndugu Washiriki
Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwahimiza wanawake kote nchini hasa wa vijijini kujiunga na VICOBA kwani vikundi hivi vimekuwa vikijaza pengo la ukosefu wa mitaji na ajira kwa wananchi kutokana na mabenki na asasi za kifedha kushindwa kutoa huduma kwa wananchi hao kwa kigezo cha kutokukopesheka. Kwa kujiunga na VICOBA leo tunashuhudia wote kuwa vikundi hivi vinakopesheka kama vikiandaliwa utaratibu maalumu kama huu tunaoushuhudia leo, kinyume na mtazamo wa taasisi nyingi za kifedha hasa mabenki kuwa vikundi hivi havikopesheki. Napenda kuishukuru Benki ya Posta kwa Kukubali kushirikiana na Serikali katika azma yake ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hongereni sana.
Ndugu Washiriki
Baada ya kusema hayo napenda kurudia kutoa wito wangu kwa wananchi wengine hasa wanawake nchini kote kuanzisha na kujiunga na VICOBA ili waweze kunufaika na huduma za Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Benki ya Posta na taasisi zingine.
VICOBA HOYEEE
ASANTENI NA NAWASHUKURU KWA KUNISIKILIZA
Mkurugenzi mkuu wa Bank ya Posta bw Sabasaba Moshingi kushoto akikabidhi hundi ya fedha kwa wanakikundi walio pewa mkopo na bank ya posta (picha zote na John Luhende )
Wana vikoba wakisikiliza kwa makini hotuba ya kaimu katibu mkuu wa baraza la uwezeshaji bi Anna Dominick
Mkurugenzi mkuu wa Bank ya Posta bw Sabasaba Moshingi kushoto mwenye kot jeusi akikabidhi zawadi kwa wanavikoba waliofanya vizuri
Post a Comment