Ads

TRC YALETA NEEMA USAFIRI WA SGR

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Shirika la Reli Tanzania (TRC)  imefanya majaribio ya Treni ya umeme ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ambao unatarajia kuanza rasmi mwezi Julai, 2024 na kuleta tija katika sekta ya usafiri kwa kuchochea shughuli za uchumi.

Katika majaribio ya usafiri wa SGR abiria walioshiriki, Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi, Wafanyakazi wa TRC, Wahariri na wanahabari pamoja na watumishi wa serikali kutoka Idara mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Februari 26, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa, amesema kuwa mradi huo unatarajia kuanza kufanya kazi mwezi Julia, 2024, huku akieleza miundombinu ya mradi wa SGR umekamilika.

Bw. Kadogosa amesema  amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.

"Leo ni muendelezo wa majaribio ya treni ya umeme ya kisasa  (SGR) tunawaambia watanzania reli yao inaelekea kuanza kutumika rasmi kama Mhe. Rais Dkt. Samia alivyoyatoa ya maagizo kuwa  mwishoni mwa mwezi wa saba tuwe tumeshaanza kutoa huduma ya usafiri huu kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma" amesema Bw. Kadogosa.  

"Tunajenga kwa vipande kuna kipande cha kwanza cha kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, kipande kingine cha pili cha kutoka Morogoro mpaka Makutupora, vipande vingine ujenzi unaendelea  kutoka Makutupora kwenda Tabora,Isaka, Mwanza na Tabora kwenda Kigoma" amesema Bw. Kadogosa.

Amefafanua kuwa hivi karibuni wamesaini mkataba wa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa SGR 

kutoka Uvinza kwenda Msongati kwa maana ya kuunganisha na Burundi baadaye itaenda mpaka DRC  Congo,"amesema Bw. Kadogosa.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi, amewatoa hofu watanzania kuhusu huduma ya umeme katika utekelezaji SGR, huku akieleza kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeingia makubaliano na TRC ili kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika.

Bw. Matinyi amesema kuwa TANESCO wametoa upendeleo katika kufanikisha huduma ya usafiri SGR ili  kuleta ufanisi katika utekelezaji wa huduma ya usafiri huo.

"TANESCO imeunganishwa umeme kutoka grid ya Taifa ambao hautakuwa na usumbufu, serikali ilivyaamua kuleta treni ya umeme ya kisasa  ilikuwa na uhakika kutakuwa umeme wa kutosha" amesema Bw. Matinyi.

No comments