Ads

Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri yafanya maandamano kuomboleza kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhamad (SAW).

Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri imefanya Maandamano ya amani jijini Dar es Salaam kuomboleza kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS) aliyeuawa kikatili huko mji wa Kerbala nchini Iraq na Jeshi la Yazid.

Siku moja kabla ya maandamano hayo jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama- Kanda ya Mashariki na Pwani iliendesha Kampeni ya Kuhamasisha Uchangiaji Damu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Ashura ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa damu hospitali.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa mchakato wa uchangiaji damu, Muzarat Chagani matarajio yao ni kukusanya unit 400 hadi 600 za chupa za damu na kwamba uchangiaji huo ni endelevu

Akizungumza na wanahabari jijini humo Imam wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri  kutoka Canada Assad Jaffar alisema siku hiyo ni kumbukumbu ya kiongozi huyo aliyejitolea kupigania maisha ya wanadamu bila ubaguzi hivyo wanaitumia kupinga ukandamizaji na unyanyasaji wa aina yeyote.

“Tunaamini katika Imam Hussein kiongozi aliyejitoa kuwapigania wanyonge tutaendelea kupinga uonevu wowote kwa kuhimiza amani na utulivu kwa waislamu wote,” alisema Imam Assad.

Alibainisha kuwa maadhimisho ya kumkumbuka kiongozi huyo ni chachu ya kuendeleza umoja, amani na utulivu bila kujali itaikadi za kidini hivyo waamini wote wa jumuiya hiyo wanatakiwa kuendelea kudumisha ushirikano na madhehebu mengine.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Ilala Omari Kumbilamoto ameziomba taasisi na jumuiya nyingine kuiga mfano wa Jumuiya hiyo kwa kujitoa kuchangia damu ili kusaidia wagonjwa wenye mahitaji.

Meya kumbilamoto alisema uchangiaji uliofanywa na taasisi hiyo umeonyesha ni kwa jinsi wanavyojitolea kusaidia watu wenye mahitaji ya damu bila kujali itikadi rangi na dini.

Naye Kiongozi wa Mkuu wa Waislam Shia  Ithnasheri Tanzania Sheikh Hemed Jalala aliwaasa waamini  wa dini zote kuvumiliana na kuendeleza amani na umoja uliopo huku akiwasisitiza kuheshimiana ili kudumisha utulivu.

Maandamano hayo yalihudhuriwa  na Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki (CCM), Ibrahim Raza, Mwenyekiti wa Khoja Shia Ithnasheri Alhaj Azim Dewji, Balozi wa Iran nchini Tanzania,Mousa Farhang pamoja na viongozi wengine wa jumuiya hiyo.

No comments