Ads

KFW Yatoa Msaada wa bilioni 32 kuzuia maambukizi ya VVU


SERIKALI ya Tanzania imesaini Mkataba wa kupokea msaada wa Euro mil 13 sawa na Sh Bilioni 32.74 kutoka Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya nchi hiyo (KFW) kwa ajili ya Mradi wa kupunguza vifo vya wakinamama, watoto chini ya miaka mitano pamoja na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika Hafla ya kusaini ya mkataba huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James alisema msaada uliotolewa ni mwendelezo wa Ujerumani kuisaidia Tanzania na kwamba hauna masharti magumu.

Alisema kuwa mradi huo ulianza 2012 ambapo katika awamu ya kwanza Serikali ya Ujerumani ilitoa Sh bilioni 25 zilizotumika kwenye mikoa iliyochaguliwa kutokana na vigezo vya kukithiri vifo wakinamama na watoto.

“ Fedha zinatolewa kama msaada hazina masharti magumu tutazipeleka kwenye mikoa husika zikasaidie kumaliza tatizo hili tunaishukuru Ujerumani kwa kuendelea kutusaidia,” alisema James.

Alibainisha kuwa katika kutekeleza mradi huo awamu ya pili Serikali ilipokea Euro mil 120 sawa na Sh bilioni 48 na kusisitiza kuwa mkataba ulisainiwa mwaka 2015 na kwamba awamu ya tatu Sh bilioni 32.4 zilitolewa.

Alisisitiza kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF) unaendelea kufadhili mradi huo kwa kuhakikisha wakinamama na watoto wanapata huduma bora za afya.

Alifafanua kuwa mradi huo ulianza katika mikoa miwili iliyochaguliwa ikiwemo Tanga na Mbeya na baadaye ikaongezwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Songwe sababu ya kukithiri vifo hivyo.

Katibu huyo alisema jumla ya wakinamama 11970,000 wamefaidika tangu mradi uanze na kusaidia kupunguza vifo hivyo kutoka 456 hadi 220 mwaka 2015 katika kila vizazi 100,000.

Pia alisema mradi huo umepokea jumla ya euro mil 46 sawa na Sh bilioni 115.86 zisizokuwa na masharti na kwamba katika miaka mine iliyopita Serikali ya Ujerumani iliahidi kuisadia nchi katika sekta ya afya, maji, utalii kiasi cha Sh bilioni 510.8

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Annika Calov alisema msaada uliotolewa ni mwendelezo wa Ujerumani kuendelea kusaidia kupunguza vifo vya wakinamama na watoto.

Alisema kuwa nchi hiyo itaendelea kutoa ushirikiano katika maeneo iliyoahidi na kwamba lengo lake ni kuona wakinamama na watoto wanapata huduma bora za afya.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NHIF, Bernard Konga alisema mwaka 2012 KFW ilikubali kutoa fedha kusaidia kupunguza tatizo hilo akibainisha msaada huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kutoa huduma bora za afya.

Konga alisema tayari fedha za msaada huo zimetumika kuboresha vituo 1,000 vya afya  ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba vilivyogharimu Sh mil 900.

No comments