Ads

JWTZ Yamwaga ajira kwa vijana wote waliojenga ukuta wa mererani

Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jenerali Venance Mabeyo amewataka vijana walioshiriki kujenga ukuta wa Mererani na hawajapata ajira wanatakiwa kuripoti katika kambi ya Jeshi Mngulani JKT siku ya September 12 mwaka huu kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Jenerali Mabeyo, amesema kuwa kuna baadhi ya vijana walioshiriki ujenzi wa ukuta wanatakiwa kufika katika kambi hiyo wakiwa na cheti walichotunukiwa baada ya kukamilika kwa mradi wa ukuta wa Mererani pamojana cheti cha kumaliza mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Amesema kuwa lengo  ni kuajiri vijana wote walioshiriki ujenzi wa ukuta kama alivyosema Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Jenerali Mabeyo ameeleza kuwa mpango wa kuajiri ni mchakato unaoendelea, hivyo vijana wanapaswa kuwa wavumilivu wakati Jeshi likiendelea na taratibu zake za kuwaajiri.

"Wapo vijana ambao walishiriki ujenzi wa ukuta wa Mererani bado hawajapata ajira,wamekuwa wakilalamika kuwa hawajaajiriwa kama Rais alivyoagiza wakati akizindua ukuta huo" amesema Jenerali Mabeyo.

Amesisitiza kuwa vijana wanatakiwa kuondokana na dhana ya kuamini kuwa kujiunga na mafunzo ya JKT umaweza kupata ajira ila fursa za ajira zinaweza kupatikana ila ni chache.

"Mafunzo ya JKT kwa ajili ya kuwajengea vijana ukakamavu, uzalendo pamoja na mafunzo ya ustadi wa maisha ili waweze kujiajiri wenyewe pindi wanapomalima mafunzo hayo" amesema Jenerali Mabeyo.

Katika hatua nyengine Jenerali Mabeyo, amesema kuwa Rais amemteua Brigedia Jenerali Charles Mbuge kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na  Meja Jenerali Martini Busungu kuwa Mkuu wa Jeshi la Akiba .

No comments