WAGONJWA WA MACHO 300 NCHINI WAFANYIWA UPASUAJI NDANI YA SIKU TANO
Mwambawahabari
Na WAJMW-DODOMA
Watu wenye matatizo ya macho takribani 700 wamefanyiwa
uchunguzi na kati ya hao wagonjwa 300 waliobainika kuwa na matatizo
ya macho wamefanyiwa upasuaji na kurejeshewa hali ya kuona vizuri.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mpango wa Huduma
za Macho kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Bernadetha Shilio wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku
ya siku ya afya ya macho duniani kilichofanyika mapema leo katika viwanja
vya Nyerere jijini Dodoma.
“Siku ya afya ya macho duniani ina lengo kuu la
kuhamasisha utekelezaji wa dira ya kimataifa ya kutokomeza upofu unaozuilika
ifikapo mwaka 2020, na kutathmini haki ya kuona kwa wote ambapo mwaka
2003 serikali ya Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani katika
kutekeleza azimio hilo”. Alisema Dkt. Shilio
Dkt. Shilio amesema Serikali ya Tanzania inashirikiana
na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya afya ya macho ikiwa na
lengo la kutoa elimu kwa jamii, kutoa huduma za uchunguzi wa macho pamoja
na kufanya upasuaji kwa wagonjwa ambao watabainika kuwa na matatizo.
Pia Dkt. Shilio ameiasa jamii ya kitanzania kuzingatia
kanuni sahihi za utunzaji wa macho ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza
na kusababisha uono hafifu na kupelekea upofu.
“Matumizi ya rangi na kope bandia kwenye ukingo
wa macho, kuvaa miwani bila kupima, kutumia dawa za mgonjwa mwingine
wa macho bila ushauri wa daktari, kutokula vyakula bora vyenye virutubisho
na kutokua na tabia ya kupima macho angalau mara moja kwa mwaka vimetajwa
kuwa visababishi vikubwa vya kuathiri afya ya macho” alisema Dkt.
Shilio.
Aidha, Dkt. Shilio amesema sambamba na huduma za
macho pia kumekua na huduma za uchunguzi na ushauri kwa magonjwa yasiyoambukiza
jijini Dodoma, jumla ya watu 400 walifanyiwa vipimo vya sukari, shinikizo
la damu na kiwango cha unene. Ambapo asilimia 3 wamekutwa na kiwango
cha juu cha sukari, asilimia 47 wamekutwa na shinikizo la juu la damu
na asilimia 50 wamekutwa na unene uliopitiliza kiwango.
Kwa upande wake Mgonjwa aliyepata huduma za macho
Jijini Dodoma Bi.Veronica Maganga ameishauri serikali kuendelea kutoa
elimu, kusogeza na kutoa huduma za macho na uchunguzi wa magonjwa mengine
karibu na wananchi ili kuzuia magonjwa yanayoweza kuleta madhara iwapo
hayatachunguzwa mapema na kutoa matibabu sahihi.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuletea huduma
hii kwani wengi tumepata matumaini ya kuona tena kwa uono mkubwa ila
wangefanya huduma hii iwe endelevu mpaka vijijini ili kuwanusuru wenye
matatizo ya macho” alisema Bi. Veronica.
Post a Comment