ZAO LA MCHIKICHI KUMALIZA UHABA WA MAFUTA NCHINI.
SEKTA
ya kilimo ni mhimili wa uchumi wa Taifa na inategemewa katika
kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025, kupitia viwanda
kwa sababu kilimo ndicho kitawezesha viwanda kwa kuvipatia malighafi.
Kutokana
na umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchini, serikali
imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha inaiboresha ili iweze kuwa na
tija na kufikia malengo iliyojiwekea.
Sekta
hiyo mbali na kuwa mhimili wa uchumi wa Taifa, pia imekuwa ikichangia
pato la mkulima mmoja mmoja, kaya na pia ni tegemeo la mapato ya fedha
za ndani na za kigeni.
Kufuatia
hali hiyo, Serikali imeweka msisitizo katika kusimamia mazao makuu
matato ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku
ambayo uzalishaji wake umeonyesha tija.
Baada
ya kupata mafanikio katika mazao hayo Serikali kwa sasa inaboresha
kilimo cha mazao ya alizeti, ufuta, michikichi ili kuzalisha mafuta ya
kula ya kutosha kwa kutumia mazao hayo na mbegu za pamba.
Itakumbukwa kwamba kila mwaka, Serikali inatumia sh. bilioni 600 kwa ajili ya kuagiza mafuta ghafi ya kula kutoka nje ili kukidhi mahitaji kwa kuwa kiwango kinachozalishwa nchini hakitoshi.
Katika
kuhakikisha kuwa jambo hilo linafanikiwa Serikali ya awamu tano
inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imeamua kuanzisha kampeni ya
kufufua zao la michikichi ili kuweza kuzalisha mafuta ya kutosha.
Akizindua kampeni hiyo mkoani Kigoma hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali
imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa
kufanya mageuzi makubwa katika zao la michikichi.
Uamuzi huo sasa umelifanya zao hilo kuwa la sita la biashara ambalo katika miaka ya l960 hadi 1970, mkoa wa Kigoma ulijipatia umaarufu kwa uzalishaji wa zao hilo.
Waziri Mkuu anasema kampeni
ya kufufua zao la michikichi mkoani Kigoma inaenda sambamba na
kuanzishwa kwa kituo cha utafiti wa zao hilo katika chuo cha Maendeleo
ya Jamii cha Kihinga kilichopo wilayani Kigoma kwa kuwa ndiko zao la
Michikichi linalimwa kwa wingi.
Anasema
zao la mchikichiki ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa nchini, hivyo
ufufuaji wa zao hilo ni kichocheo cha viwanda kwa kuwa kutakuwa na
uhakika wa upatikanaji wa malighafi na kuvutia wawekezaji.
Waziri
Mkuu anabainisha kuwa licha ya kuwepo kwa michikichi mingi nchini
lakini uzalishaji wake unafanyika kwa njia za kienyeji, hivyo Serikali
imedhamiria kuboresha kilimo hicho kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili
liweze kuleta manufaa makubwa kwa Taifa na wakulima.
Anasema
kuwa Serikali haiwezi ikaendelea kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza
mafuta ya kula kutoka nje wakati uwezo wa kulima michikichi na
kuzalisha mafuta ya mawese kwa wingi tunao.
Anasisitiza
kwamba inawezekana kujitosheleza kwa mafuta ya kula kwa sababu Tanzania
ina ardhi ya nzuri yenye rutuba na watu ambao kilimo ndiyo shughuli
kubwa wanayoitegemea kujipatia kipato.
Waziri
Mkuu anasema ili kufanikisha kampeni hiyo ni lazima viongozi wa
Serikali wabadilike na wawafuate wakulima kwenye maeneo ya vijijini
wakawaelimishe na kuwashauri namna bora ya kulima zao hilo.
“Tunataka
kufanya mageuzi makubwa ya zao la michikichi, tunataka tuzalishe mafuta
ya kutosha kutokana na zao hili, hivyo tuanze kupanda michikichi mipya
na kuiondoa ile ya zamani kwa awamu,”.
Kadhalika,
Waziri Mkuu anasema Serikali inataka kuona mabadiliko ya zao hilo,
hivyo amewaagiza Maafisa Ugani katika maeneo yote wanayolima michikichi
wafualitie maendeleo ya zao hilo kwa ukaribu zaidi.
Waziri
Mkuu amewataka wananchi wote wa mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa mingine
inayolima michikichi, wahakikishe wanapanda michikichi kwa wingi
kuanzia kwenye makazi yao na kwenye mashamba yote wanayolima mazao
mengine ili kuongeza uzalishaji.
“Serikali
imefanya maamuzi ya kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula
nchini, kila mmoja lazima awajibike katika kuinua zao la michikichi ili
tuweze kuzalisha mafuta ya kutosha,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itafuatilia kwa umakini kuhakikisha zao la
michikichi linalimwa kwa wingi na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa
ujumla. “Tutumie zao hili kama fursa ya kujikwamua na umasikini pamoja
na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini,”.
Pia
amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote nchi kuhakikisha mashamba ya
wananchi yanapimwa na wahusika kupewa hati ili ziwawezeshe kupata
dhamana ya mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha na kuwekeza
kwenye kilimo.
Waziri
Mkuu anabainisha kuwa halmashauri zinazolima michikichi viongozi wake
wanatakiwa kuanzisha vitalu vya miche ya zao hilo na watakaoshindwa
kuanzisha vitalu hivyo pamoja na kuhamasisha kilimo cha michikichi
kwenye maeneo yao wajitathimini mwenyewe.
Anaongeza
kuwa kuanzia sasa mkoa huo uhakikishe miche ya michikichi inapandwa
katika maeneo yote yakiwemo ya pembezoni mwa barabara, katika mashamba
ya shule za msingi na sekondari, kambi ya JKT na kwenye magereza na
kwenye makazi ya wananchi.
Hata
hivyo Waziri Mkuu alitoa angalizo kwa wawekezaji watakaowekeza katika
kilimo cha michikichi kutoanzisha migogoro na wananchi watakaowakuta
katika maeneo yao na badala yake washirikiane nao vizuri kwa sababu
migogoro haina tija kwao na kwa wananchi.
Waziri Mkuu anasema Serikali
imeliteua Gereza la Kwitanga lililopo wilayani Kigoma kuwa kituo kikuu
cha uzalishaji wa zao la michikichi nchini kwa kuwa tayari lilishaanza
kujishughuliza na kilimo cha zao hilo.
Ameuagiza
uongozi wa gereza hilo kuongeza nguvu katika uzalishaji wa michikichi
kwa kupanua mashamba na kuongeza askari wenye ujuzi wa kilimo cha
michikichi.
Kwa upande wake,Mkurugenzi
Mtendaji wa Trade Mark East Africa, Bw. John Ulanga alisema walifanya
utafiti kuhusu zao la michikichi na walibaini kuwa kuna
soko kubwa la mafuta ya mawese ndani ya nchi yetu, pamoja na nchi za
jirani ila uzalishaji wa mafuta hayo ndani ya nchi bado ni mdogo sana.
Alisema hali hiyo inachangiwa na kuwepo kwavikwazo
vichache vinavyokwamisha ongezeko la uzalishaji wa ndani, ambavyo ni
matumizi ya teknologia hafifu katika kilimo cha mchikichi, na
ukamuaji wa mafuta ya mawese.
Pia ukosefu wa miundombinu na usafiri, ukosefu
wa maghala ya kukusanyia matunda ngazi ya wilaya, na badala yake
mkulima mmoja mmoja anahangaika kupeleka kwa mteja hivyo kumuongezea
gharama, ukubwa wa gharama za usafiri kutoka shambani mpaka sokoni.
Naye,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB), Bw. Josephat Faustine alisema kilimo cha zao la michikichi kina
faida kubwa na kinawekezeka, hivyo wao wataanisha maeneo yote yanayofaa
kuwekeza.
Pia
Mkurugenzi huyo wa TADB alisema benki yao inauwezo wa kutoa mikopo ya
mitaji kwa vituo vya uzalishaji mbegu za zao la michikichi na kumaliza
changamoto ya upatikanaji wa mbegu, hivyo ni muhimu kwa wakala wa mbegu
kuchangamkia fursa hiyo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 2, 2018.
Post a Comment