TABORA KUZINDUA KAMPENI YA FURAHA YANGU MJINI NZEGA SIKU YA IJUMAA
NA TIGANYA VINCENT
TABORA
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri
anatarajia kuzindua rasmi kampeni ya kimkoa ya upimaji virusi vya Ukimwi VVU inayojulikana
kwa jina la ‘Furaha Yangu’ yenye lengo la kuhamasisha huduma za kupima VVU na
kuanza ARV mapema hasa kwa wanaume.
Kampeni hiyo itakayozinduliwa Agosti
3 mwaka huu mjini Nzega, inalenga kuwaleta wanaume kwenye huduma kutokana na
wengi wao kuwa waoga kuzifikia.
Kaimu Mganga MKuu wa Mkoa wa Tabora
Dkt. Kevin Nyakimori alisema kampeni hiyo inahamasisha mkakati mpya wa Serikali
wa upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV mapema kwa wale watakaokutwa na VVU.
Alisema lengo lake ni kuchochea
mabadiliko ya tabia ndani ya jamii ili kuongeza idadi ya Watanzania walio
katika mazingira hatarishi wajitokeze kupima na kujua hali za afya zao katika
suala zima la VVU.
Dkt Nyakimori alisema kampeni hiyo itazinduliwa katika viwanja wa
Parking mjini Nzega na itakuwa na siku mbili za kutoa huduma za afya bila
malipo ikiwemo huduma ya upimaji wa VVU kuanzia Agosti 3 hadi tarehe 4 Mwezi
huu.
Alisema kampeni hiyo ni
muhimu kwa Mkoa huo kwani matokeo yanaonyesha kiwango cha
maambukizi ni asilimia 5.1 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 ambacho
ni kiwango cha juu ya kile cha kitaifa 4.7.
Kaimu Mganga huyo wa Mkoa alisema
juhudi za serikali ni kufikia malengo ya Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Ukimwi (UNAIDS) ni kutaka kutambua watu wote
wanaoishi na VVU kutambua hali zao na watue ARV ili waweze kufubaza
virusi hivyo
Dkt. Nyakimori alizitaja huduma
ambazo zitatolewa ni upimaji wa VVU, huduma za uzazi wa mpango, uchunguzi wa
saratani ya shingo ya kizazi na matiti, uchunguzi wa maambukizi ya kifua kikuu
, uchunguzi wa magonjwa yasiyo ambukizwa na uchangiaji damu.

Post a Comment