Ads

TAAFIYA KUHUSU HAKI ZA BINADAMU KATIKA BIASHARA YAZINDULIWA DAR


mwambawahabari
TUME ya Haki za binadamu na Utawala Bora, imevitaka vyombo vinavyohusika na sheria kutekeleza na kusimamia haki za binadamu katika biashara . 


Mwenyekiti wa Tume ya haki za binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanguda(katikati)  akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa Uchunguzi wa taarifa wa haki za binadamu katika biashara nchini  leo, kushoto ni Kamishna wa tume hiyo,  Muhammed Hamis Hamad na Ofisa Uchunguzi Mwandamizi,  Jovina Muchunguzi. (picha na John Luhende)

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam  na Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanguda alipokuwa akizindua mpango wa uchunguzi wa taarifa wa haki za binadamu katika biashara. 
Amesema kuzinduliwa kwa taarifa hiyo utawezesha kuangalia biashara zinazozingatia haki za binadamu nchini. 

"Mwaka 2013 serikali iliandaa mpango kazi wa haki za binadamu nchini ambao unaratajia kukamilika Disemba mwaka huu ambao umeainisha masuala ya namna ya kusimamia, kulinda,  kuheshimu na kutetea haki za binadamu katika kipengele cha biashara, "amesema. 
Amesema katika biashara kipengele cha haki za binadamu hakikutekelezwa katika kipindi cha miaka 4 iliyopita na kuamua kuandaa mpango kazi utakaosimamia haki za binadamu katika biashara. 

Amesema umoja wa mataifa umekubaliana na malengo endelevu kuzingatia haki katika masuala ya biashara, maendeleo ya ukuaji wa uchumi, haki za kijamii ambazo zinaguswa na biashara. 
Ameongeza umoja wa mataifa ulizitaka kampuni binafsi  zinapowekeza ziweze kuisaidia   jamii kwani ilionekana kujitolea katika huduma za kijamii haitoshi. 

Amesema watu wamekuwa na dhana potofu kwamba kampuni haihusiki katika uvunjaji wa haki za binadamu nakubainisha kwamba kampuni inaweza kuhusika na zinaweza kuchukuliwa hatua za kisheria ilimradi taasisi zinazohusika na utekelezaji wa Sheria ufanye hivyo.  
"Wasikubali udhaifu huo ni lazima haki za binadamu zifuatwe.. .. Sheria zipo na mara nyingine utekelezaji wake ni hafifu, "amesema. 

Kwa upande wake ofisa uchunguzi  Mwandamizi wa tume hiyo, Jovina Muchunguzi amesema katika taarifa hiyo waliibua changamoto zinazoonesha uhalisia ambayo yamepangiwa utekelezaji wake. 

"Tunaamini tutafika kwenye kutatua changamoto ambazo zimelengwa hasa kwenye Viwanda, uchimbaji madini, kilimo, utalii na biashara, "amesema. 

Akizungumzia athari ambazo wameziona katika uchunguzi huo, Kamishna wa tume hiyo,  Muhammed Hamis Hamad amesema changamoto ipo kwenye  sekta ya utalii. 

" Tumeangalia katika sekta ya utalii Zanzibar, lakini tumeangalia athari kwa binadamu na changamoto zipo si kwa watembeza watalii tu lakini hata kimazingira, "amesema. 

Amesema kumekuwa na uharibifu wa mazingira katika sehemu za makazi ya watu kwa kujengwa hoteli huku miundombinu ikiwa haiboreshwi. 

 " Lazima tuangalie lakini pia kuna uvunjifu wa haki za binadamu kwa watu kupata matatizo, ghasia, takataka masuala ya usalama ingawa utalii unachangia kwenye pato la taifa, "amesema.

Ameongeza kuwa uzinduzi wa uchunguzi huo ni mpya  nchini huku akibainisha kutokuwepo kwa sheria ya makampuni kuisaidia jamii. 

" Nchi zingine ni lazima kampuni iliyowekeza kuwa na wajibu  wa kuisaidia jamii... Lakini sasa hivi makampuni hufanya kwa hiari hayalazimishwi kisheria na ndiyo wajibu wao kuisaidia jamii, "amesema. 

No comments