JKCI YAOKOA SHILINGI MILIONI 174 KWA KUFANYA UPASUAJI WA MOYO NDANI YA NCHINI.
Na: Lilian Lundo
mwambawahabari
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha shilingi Milioni 174 kwa kuwafanyia upasuaji wa moyo wagonjwa 6 katika taasisi hiyo.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Upasuaji JKCI ambaye pia ni Daktari Bingwa Upasuaji wa Moyo Dkt. Bashir Nyangasa wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyotokana na upasuaji huo.
“Kwa mwaka 2017 tumeanza kwa kufanya kambi ya kwanza ya upasuaji kwa kushirikiana na timu ya wataalamu kutoka hospitali ya Apollo, Bangalore ya nchini India na kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa sita (6) kati ya hao wanaume ni wanne na wanawake wawili,” alifafanua Dkt. Nyangasa.
Aliongeza kuwa badala ya kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi, wamewaleta madaktari wa Apollo nchini ambapo imesaidia kupunguza gharama wakati huo huo wataalamu wa JKCI wameweza kujifunza aina mpya ya upasuaji wa magonjwa wa moyo.
Dkt.Ngangasa alifafanua kuwa kama Serikali ingewasafirisha wagonjwa hao 6 kwenda kupata matibabu nje ya nchi gharama ya shilingi milioni 174 ingetumika ambapo kwa kuwafanyia wagonjwa hao hapa nchini gharama ambayo imetumika haizidi shilingi milioni 60.
Upasuaji uliofanyika ni upasuaji wa kuvuna mishipa ya damu mguuni na kuipandikiza katika mishipa ya moyo iliyokuwa imeziba (CABG-Coronary Artery Bypass Graft) ambapo upasuaji huo uliweza kufanyika bila kutumia mashine ya mapafu na moyo.
Aliongeza kuwa upasuaji mwingine uliofanyika ni wa kubadilisha milango ya moyo (Valves) ambayo haikuwa inapitisha damu vizuri. Pia mgonjwa mmoja amefanyiwa upasuaji wa milango miwili ya moyo ambayo iliharibika sana, milango hiyo ilibadilishwa na kupanuliwa kwa kishina cha mshipa mkubwa wa moyo kwa kutumia mfuko wa moyo (Aorta).
Kwa upande wa Mshauri Mwandamizi kutoka hospitali ya Apollo Dkt. Sathyaki Nambala alisema kuwa ni mara ya nne amekuja Tanzania, lakini kwa sasa amekuta kuna jengo jipya kwa ajili ya wagonjwa wa moyo ambalo lina vifaa vyote muhimu na vya kisasa kwa ajili ya upasuaji wa moyo.
Alongeza kuwa hatua hiyo imesaidia Serikali ya Tanzania kupunguza kiasi kikubwa cha fedha kwa kuwafanyia wagonjwa upasuaji ndani ya nchi badala ya kuwapeleka nje ya nchi.
Vile vile, Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo JKCI Peter Kisenge alisema kuwa Taasisi hiyo inategemea kupokea madaktari kutoka Afrika na Saudi Arabia kwa ajili ya upasuaji wa kutanua mishipa ya moyo iliyoziba, kutanua milango ya moyo iliyoziba na kuziba matundu ya moyo.
Kambi ya madaktari wa Afrika itakuwepo katika Taasisi hiyo kuanzia tarehe tarehe 23 mpaka 29 mwezi huu, ambapo wagonjwa 15 watafanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua(Catheterization Procedure).
Kambi ya madaktari bingwa kutoka Saudi Arabia watafanya upasuaji wa bila kufungua kifua (Device Closure) ambapo wagonjwa zaidi ya 55 wenye umri kuanzia miaka 12 na kuendelewa watafanyiwa upasuaji kuanzia tarehe 04/02/2017.
Aidha Madaktari wote nchini na wanachi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani wenye wagonjwa wa moyo ambao wana matatizo hayo ya moyo wameombwa kuwatuma wagonjwa katika Taasisi hiyo ili kupatiwa matibabu. Pia wanaweza kuwasiliana na Dkt. Kisenge kuitia namba 0713 236 502 au 022-2151379.
Post a Comment