SERIKALI imezindua ripoti ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2015/16
Na. Eliphace Marwa
SERIKALI imezindua ripoti ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2015/16 mapema hii leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni awamu ya tatu katika ugonjwa wa malaria ambapo ripoti imeonesha kupungua kwa vifo vya watoto wadogo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mgeni Rasmi ambaye pia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuaanda ripoti iliyoonesha Taifa kupiga hatua katika utoaji wa huduma ya mama na mtoto.
Waziri Ummy ameeleza kuwa ripoti hiyo itaisaidia Wizara ya Afya na serikali kwa ujumla katika kutathmini na kufuatilia utekelezaji wa mipango endelevu katika huduma za afya hapa nchini ili kuboresha utoaji wa huduma ambazo ripoti imeonesha haikufanya vizuri kutokana na changamoto mbalimbali ambazo ripoti imezibainisha.
“Ripoti hii imeonesha kuwa bado kuna changamoto katika mimba za utotoni kwani zimeongezeka ukilinganisha na mwaka 2010 ambapo watoto 23 kati ya mia moja walipata mimba wakiwa na umri mdogo ukilinganisha na sasa watoto 27 kati ya mia moja hupata mimba katika umri mdogo hivyo kuna haja ya jamii kuelimishwa juu ya madhara ya mimba za utotoni”, alisema Waziri Ummy.
Aliongeza kuwa kuna haja ya serikali kuangalia upya sheria ya kuruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo endapo akipata mimba akiwa shuleni kwani kumzuia kuendelea na masomo ni kupoteza nguvu kazi ya taifa na kuikwamisha serikali kufikia malengo yake ya uchumi wa viwanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa iwapo huduma za afya zitaboreshwa zitapelekea ukuaji wa uchumi kwasababu ya uwepo wa nguvu kazi ya uhakika na kuongeza uzalishaji kwa Taifa.
“Wananchi wakiwa hawana afya ya kutosha na kuugua mara kwa mara uchumi wa nchi yoyote Duniani hupungua kasi ya ukuaji kwa kuwa rasilimali fedha ambazo zingeelekezwa kukuza sekta nyingine hupungua na hata nguvu kazi kupungua” alisema Dkt. Chuwa.
Aidha Dkt. Chuwa aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 inatamka kuwa yeyote atakaepotosha Takwimu hizi kwa makusudi atachukuliwa hatua za kisheria kupitia kifungu cha 37 cha sheria hiyo.
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa mwaka 1991-92 ulionyesha kuwa katika kila watoto 1000 wanaozaliwa hai, watoto 141 walikuwa wakifariki kabla ya kufikia umri wa miaka mitano ila utafiti huu umebaini kuwa ni watoto 67tu ndiyo wanaofariki kati ya watoto 1000.
Post a Comment