NEC YATOA SOMO KWA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA DIMANI ZANZIBAR.
|
Viongozi wa vyama vya
Siasa vitakavyoshiriki uchaguzi mdogo katika jimbo la Dimani wakifuatilia mada
wakati wa mkutano wao na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mjini Zanzibar leo.
Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damiani Lubuva (kushoto) akizungumza na baadhi ya
viongozi wa vyama vya Siasa mjini Zanzibar mara baada ya kumalizika kwa mkutano
wa Tume na Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo jimbo la Dimani mjini
Zanzibar.
Mkurugenzi wa Huduma
za Sheria wa NEC Bw. Emmanuel Kawishe akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya
kisheria leo wakati wa Mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na
viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani. PICHA/Aron Msigwa –
NEC.
Na. Aron Msigwa –
NEC, Zanzibar.
Mwambawahabari
Mwambawahabari
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) imevitaka Vyama vya Siasa na wagombea watakaoshiriki Uchaguzi
mdogo katika jimbo la Dimani visiwani
Zanzibar kuzingatia Sheria , Kanuni,
Taratibu na Maadili ili Uchaguzi huo uwe huru na wa haki na kuwawezesha
wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
Kauli hiyo imetolewa
leo mjini Zanzibar na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu
Damiani Lubuva wakati akizungumza na Viongozi 19 wa vyama vya Siasa
waliohudhuria mkutano wa maandalizi ya kufanikisha Uchaguzi mdogo wa jimbo la
Dimani utakaofanyika Januari 22, 2017.
Amewataka viongozi wa
Vyama vya Siasa waliohudhuria mkutano huo waendelee kudumisha hali ya amani na
Utulivu wakati wa kampeni za vyama vyao zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni pia kutoa ushirikiano kwa Waratibu na
Wasimamizi wa Uchaguzi huo.
“Ni matarajio ya Tume
kuwa, Vyama vya Siasa vitatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha
uchaguzi wetu katika jimbo la Dimani unakuwa
Huru na wa Haki, lengo hili litafanikiwa tu iwapo vyama na wagombea wote
watazingatia na kufuata sharia na maelekezo na maadili ya Tume” Amesisitiza
Jaji Lubuva.
Amevitaka vyama vyote
vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo wakati wa kampeni vijikite katika kuelezea
Sera zao na si vinginevyo pia kuepuka matumizi ya lugha ambazo zinaweza
kusababisha machafuko.
Ameeleza kuwa katika
kufanikisha uchaguzi huo kila Chama cha Siasa kina haki ya kuteua Wakala mmoja
kwa kila kituo cha kupigia kura ili kuongeza uwazi katika uchaguzi huo na
kuongeza kuwa mawakala hao watapangwa kwenye vituo vilivyo ndani ya Shehia
wanakoishi ili waweze kuwatambua wapiga kura katika eneo husika.
“Vyama vyote lazima
muhakikishe kuwa mawakala mnaowateua wanaelewa hatua zote muhimu za uchaguzi
vituoni kuanzia hatua ya kwanza ya kufungua kituo hadi kutangaza matokeo”
Amesisitiza.
Aidha, Mhe. Lubuva
amewasisitiza viongozi wa vyama hivyo watambue kuwa watu watakaopiga kura
Januari 22,2017 ni wale walioandikishwa kwenye daftari la kudumu Wapiga Kura
ambao watakuwa na Kadi za kupigia kura na si vinginevyo.
“ Naomba ninyi
viongozi wa vyama vya Siasa muwakumbushe wanachama wenu walio na sifa na kadi
za kupigia kura wajitokeza siku ya kupiga kura, pia muendelee kuwahamasisha
wajitokeze kwa wingi kupiga kura
siku hiyo” Amesema Mhe. Lubuva.
Katika hatua nyingine
Mhe. Lubuva amewakumbusha viongozi hao kuwa wananchi wakishapiga kura hawapaswi
kubaki katika eneo la vituo vya kwa kuwa vyama hivyo vitakuwa na Mawakala ndani
ya vituo hivyo na kuongeza kuwa ni
marufuku kwa mgombea , Chama cha Siasa au Wakala kufanya kampeni Siku ya
Uchaguzi kwani mwisho wa kupiga kampeni ni siku moja kabla ya siku ya uchaguzi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhan akizungumza
na viongozi wa vyama hivyo amesema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea
vizuri huku akisisitiza kuwa ni matarajio ya Tume kuwa Vyama vyote vitazingatia
Katiba, Sheria, Kanuni, Maelekezo na taratibu zote halalali zitakazotolewa na
NEC.
Amewataka viongozi wa
vyama hivyo kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wapiga kura wao kuepuka kufanya
vitendo vya vurugu au viashiria vyovyote vya vurugu au uvunjifu wa amani ili
wananchi wote waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka.
Ametoa wito kwa
wananchi wa jimbo la Dimani walioandikishwa kupiga kura wajitokeze kwa wingi
Januari 22, 2017 kwenda kupiga kura ili kufanikisha uchaguzi huo.
Kuhusu kampeni za
vyama hivyo amesema kuwa zitaanza Desemba 23, 2016 hadi Januari 21, 2017 na
kuvitaka vyama hivyo viwasilishe ratiba zao za kampeni kwa Msimamizi wa
Uchaguzi wa jimbo hilo ili viweze kukubaliana ambapo kampeni zitakua zinaanza
saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni.
Kwa upande wao
viongozi wa vyama vya Siasa waliohudhuria mkutano huo kutoka vyama 19 wakizungumza
kwa nyakati tofauti wameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutekeleza
majukumu yake kwa mujibu na kuahidi kutoa ushirikiano kwa waratibu na
wasimamizi wa uchaguzi huo.
Viongozi waliohudhuria
mkutano huo mjini Zanzibar wanatoka katika vyama vya ACT WAZALENDO,ADA, ADC,AFP, CCK, CCM,
CHADEMA, CUF, Demokrasia Makini, DP, NCCR –MAGEUZI, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP,
UMD, UPDP na CHAUMA.
Post a Comment