Ads

MADEREVA 44WAMABASI YA ABIRIA YAENDAYO MIKOANI WAKAMATWA MKOANI PWANI





Mwambawahabari

Madereva  wapatao 44 wa mabasi ya abiria yaendayo mikoani,wamekamatwa na askari wa usalama barabarani mkoani Pwani,kutokana na makosa mbalimbali ya barabarani.

Sambamba na hilo,kitengo cha usalama barabarani mkoani hapo,kimetoa onyo  kwa baadhi ya madereva wenye tabia ya kutoa lugha chafu na kuwatishia askari wa usalama barabarani pindi wanapokamatwa na kutakiwa kulipia faini.

Kaimu kamanda wa usalama barabarani mkoani hapo,mrakibu wa  polisi ASP Salumu Morimori ,amesema madereva hao wamekamatwa kufuatia ukaguzi maalum unaofanywa katika barabara kuu Chalinze -Segera na Dar es saalam -Morogoro.


Ameeleza kwamba zoezi hilo ni  endelevu likiwa na lengo la  kuzuia ajali hasa  katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa  mwaka.

Kamanda Morimori ameeleza ,zoezi hilo  lilianza barabara  ya kwenda Kusini ambayo ni  mkoa wa  kipolisi Temeke kwa kushirikiana na wilaya ya Mkuranga  Pwani.

Amesema zoezi hilo  limeendelea katika barabara  ya Morogoro, ambayo ni kutoka Kibaha hadi Bwawani  mpakani mwa Pwani  na Morogoro,  na Chalinze  hadi  Manga mpaka wa Tanga na Pwani.

Amefafanua, madereva hao 44 walikamatwa siku moja pekee ambapo kati yao madereva 37 walitozwa faini za papo kwa papo  na madereva saba ambao waliokutwa na makosa hatarishi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo,kamanda Morimori ametoa onyo  kwa baadhi ya madereva wenye tabia ya kutoa lugha chafu na kuwatishia askari wa usalama barabarani pindi wanapokutwa na makosa na kutakiwa kutozwa faini.

Amesema endapo dereva  ana malalamiko ni  vizuri akafuata taratibu kwani viko vitengo maalumu vya kushughulikia malalamiko na huko ndiko dereva   atakwenda kupata haki badala ya kutumia lugha za udhalilishaji kwa askari polisi.

Kamanda huyo amesema  ili dereva awe  salama barabarani anatakiwa kutii sheria bila shuruti kwa kuendesha kwa kuzingatia alama za barabarani.

No comments