Ads

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM YA DSM LANASA MTANDAO WA WEZI HATARI DAR


Na Maria Kaira 
mwambawahabari
Kikosi Maalum cha kupambana na wizi wa kutumia silaha na wizi wa kutumia nguvu cha Polisi Kanda Maalum Dar es salaam imefanikiwa kukamata watuhumiwa hatari 22 kwa makosa ya kuwapora wenye magari na wapita njia kwenye taa za kuongezea magari.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamishna wa kanda hiyo Saimon Sirro amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakijiunda kwenye vikundi na kuanza kuwanyang'anya watu waliopo katika magari na watembea kwa miguu mali zao.

Kamishna Sirro amesema baadhi ya watuhumiwa ni pamoja na Ayubu Amri (19) mkazi wa Mtoni Mtongani, Shabani Fadhili (18) mkazi wa Keko Toroli, Herman Francis (26) mkazi wa Keko Magurumbasi na wenzao wengine saba.


" karika mahojiano watuhumiwa wamekiri kujihusisha na makosa ya unyang'anyi kwa kutumia silaha na kutumia nguvu, pia uchunguzi wetu wa awali umebaini mtuhumiwa Herman Francis anakabiliwa na tuhuma za mauaji ambapo machi 20 mwaka huu alimchoma mtu kisu na kutoroka kusiko julikana" amesema

Pia amesema Desemba 12 askari wakiendelea na msako kwenye mataa ya Veta Chang'ombe waliwakamata watuhumiwa 12 kwa makosa ya wizi katika magari, Sande Kassim(18) mkazi wa Keko Toroli,Emanuel Abeli (21) mkazi wa Keko Toroli, Paulo Abeli(18) mkazi wa Keko Mwanga, Jafari Nyerere (22) mkazi wa keko Mwanga Hamisi Salum (22) mkazi wa Keko Mwanga, Hemedi Idrisa(22) mkazi wa keko Magurumbasi na wenzao wengine sita.

Pamoja na hayo kanda hiyo imeweza kukusanya sh 341,370,00 kupitia tozo mbalimbali za makosa  ya usalama barabarani kuanzia Desemba 8 hadi Desemba 13 mwaka huu na kuweza kuiingizia serikali Mapato ya ndani.

" Madereva wanatakiwa kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka ili kuepusha ajali zisizo za lazima watakao bainika kukiuka sheria za usalama barabarani watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa pamoja na kutozwa tozo na kupelekwa mahakamani" amesema

No comments