Ads

Shule ya Msingi Nyarugusu yaanzisha Kamati ya kudhibiti utoro


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Geita
Mwambawahabari
Shule ya Msingi Nyarugusu iliyopo mkoani Geita imeanzisha kamati ya kudhibiti utoro wa wanafunzi ikiwa ni njia moja wapo ya kuwazuia kwenda kufanya kazi katika migodi iliyopo mkoani humo.

Maamuzi hayo yametolewa na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Peter Kitagira alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya mchango wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na Shirika la Plan International. 

Kitagira amesema kuwa wameamua kuchukua maamuzi hayo baada ya kugundua kuwa asilimia kubwa ya watoto wa mkoa huo wanaacha shule na kukimbilia kufanya kazi za migodini kwa ajili ya kujitafutia kipato bila kufahamu madhara ya shughuli hizo.

“Hali ya utoro inaongezeka kwa kasi na ndio maana tumeamua kuanzisha Kamati ya Kudhibiti Utoro wa wanafunzi, kamati hiyo inafanya mawasiliano ya karibu na wamiliki wa migodi ili kuhakikisha hakuna mtoto chini ya umri wa miaka 18 atakayeajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi kwenye maeneo hayo”, alisema Kitagira.

Kitagira ameitaja sababu nyingine inayosababisha kushuka kwa mahudhurio ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kuwa ni hali duni ya maisha inayosababisha wazazi kuwaacha watoto majumbani wakilinda nyumba ili wao wakatafute fedha za kujikimu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati wa Shule hiyo, Philip Edward amesema kuwa ni vigumu sana kuwaelimisha wazazi juu ya athari za watoto kufanya kazi migodini au kuwaacha nyumbani wakilinda nyumba na kulea wadogo zao kwa sababu hawana njia nyingine ya kujipatia kipato zaidi ya kufanya kazi hizo.

“Ili kupunguza utoro shuleni hapa, kamati ya shule ilifanya kikao na wazazi ambapo tulikubaliana kutoa kiasi cha shilingi mia tano kama adhabu kwa kila mwanafunzi ambaye hatokuja shuleni lakini muda mwingine tunawahurumia wazazi kwani kipato chao ni cha shida sana”, alisema Edward.

Naye Mwalimu wa shule hiyo, Mathias Kato ambaye pia ni mlezi wa watoto wanaohudumiwa na shirika la Plan International amelishukuru shirika hilo kwa jitihada zao wanazozifanya katika kupinga ajira za watoto migodini kwa sababu umechangia kiasi kikubwa kuongeza mahudhurio ya  wanafunzi shuleni hapo.

Ametoa ushauri kwa Serikali na mashirika mengine kuangalia namna ya kuwasaidia wazazi wenye kipato duni wanaoishi katika maeneo ya migodi kwa sababu ukosefu wa kipato kwa wazazi ndiyo chanzo cha watoto kutoroka shule na kwenda kujitafutia ridhiki migodini.

No comments