WAHALIFU 71 WAKAMATWA NDANI YA WIKI GONGO LA MBOTO.

Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabariblog
Jumla ya wahalifu 71 wamekamatwa
ndani ya siku 7 katika maeneo mbalimbali katika Kata ya Gongo la mboto,Wilaya
ya Ilala, Jijini Dar es Salaam wakiwa na kete za bangi pamoja na madumu ya
pombe aina ya gongo.
Idadi hiyo imetajwa leo Jijini Dar
es salaam na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi, Bw. Lucas Mkongya alipokua
akifafanua juu ya malalamiko ya wananchi wa Gongo la Mboto kuhusu uhalifu
uliokithiri katika maeneo hayo pamoja na jitihada wanazozichukua katika
kuzuia uhalifu huo.
“Kweli uhalifu upo na kila siku
tunajitahidi kufuatilia maeneo yote ya Gongo la Mboto. ndani ya siku saba
kuanzia Aprili 14 hadi 20 mwaka huu tumekamata jumla ya kete za bangi 640
pamoja na lita 90 za pombe aina ya gongo”alisema Kamishna Msaidizi Mkongya.
Kamishna Msaidizi Mkongya
amesisitiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za
wahalifu pia amewaomba wananchi wajitahidi kuunda ulinzi shirikishi
utakaosaidia kulinda maeneo yao kwa sababu polisi pekee hawawezi
kulinda kila nyumba.
Aidha, Kamishna Msaidizi Mkongya
ametoa rai kwa wazazi kutoa malezi mazuri kwa watoto wao kwa kuwa asilimia
kubwa ya wezi wa maeneo hayo ni watoto wao wenyewe.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
walinzi shirikishi wanajitahidi kufanya doria kila siku katika maeneo
mbalimbali Jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa na
kuchukuliwa hatua stahiki.
Post a Comment