NAIBU WAZIRI JAFO AWATAKA WATENDAJI KUTEMBELEA MAENEO YAO YA KAZI.
Na Rebecca Kwandu
mwambawahabariblog
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuwa na utaratibu wa kutembelea maeneo yao ya kazi mara kwa mara ili kujionea
hali halisi na kutatua kero zilizopo.
Akizungumza na walimu wa shule ya msingi Nzuguni B. wakati wa
ziara aliyoifanya kutembelea shule hiyo na shule ya sekondari Nzuguni A.,
Mhe. Jafo alisema watumishi hawawezi kufanya kazi kwa ubora iwapo watakuwa
hawatembelei na kukagua maeneo yao ya kazi.
“ Kumekuwa na uzembe kwa Wakuu wa Idara kutokusikiliza matatizo ya
chini, kutowatembelea watumishi waliopo chini yetu inawasababishia kukosa
mahali pa kusemea shida zao na kuchanganyikiwa. Ni vizuri kuwa na utaratibu wa
kuwatembelea watumishi tunaowaongoza ili kujua shida zao na kuzitatua.
Alisisitiza Mhe. Jafo.
Aidha, aliwataka walimu wa shule za msingi Nzuguni B na Shule ya
sekondari Nzuguni A kuweka utaratibu wa kuweka malengo na kujipima kuona
walichokifanya ili kupata matokeo tarajiwa.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Nchi Jafo ametoa Mabati 164
ili kuchangia ujenzi wa Madarasa ya shule ya msingi Nzuguni B iliyopo kata ya
Nzuguni katika halmashauri ya Mji wa Dodoma.
Mhe. Jafo alitoa Mabati hayo baada ya kufanya ziara ya kutembelea
shule hiyo ili kujionea hali halisi ya maendeleo yake ikiwa ni moja ya taratibu
alizojiwekea za kutembelea maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na Ofisi ya
Rais-TAMISEMI ili kujionea changamoto mbalimbali zilizopo katika utoaji wa
huduma na kuzitafutia ufumbuzi.
Katika ziara hiyo Mhe. Jafo alikuta Idadi kubwa ya watoto
walioandikishwa kujiunga na darasa la kwanza hali iliyopelekea kukosekana kwa
vyumba vya kutosha kwa ajili ya kujifunzia wanafunzi ambapo kwa kutatua kero
hiyo, shule hiyo imeanza ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwa upande wake
alichangia bati 164 ili kuwezesha madarasa hayo kukamilika.
Post a Comment