MAFANIKIO YA ZIARA YA WAFANYABIASHARA WA OMAN NCHINI YAELEZEWA

Na: Immaculate Makilika
mwambawahabariblog
Tanzania na Oman zimesaini mkataba wa
makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania Chambers of Commerce na
Oman Chambers of Commerce ili kuanzisha
Kampuni ya Oman Tanzania Investment (OTIC) kwa lengo la kutafuta fursa za
uwekezaji zilizoko Tanzania na Oman.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Bibi. Mindi
Kasiga amesema kuwa mkataba huo ni matokeo ya ziara ya
siku tatu ya Waziri Viwanda na biashara wa Oman , Dkt. Ally Mohamed Al
Sunaidy, pamoja na ujumbe wa wafanyabiashara 108 na maafisa wa
Serikali ya Oman iliyofanyika nchini mwezi Aprili mwaka huu.
Amesema lengo la ziara hiyo lilikua
kuwawezesha wafanyabishara wa Oman na Tanzania kushiriki
kongamamo la biashara la uwekezaji lililowawezesha wafanya bishara hao kubaini
fursa za uwekezaji zilizoko nchini Tanzania na
Oman.
Amesema tayari Serikali
ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera
kilichopo mjini Morogoro ambacho kitazalisha tani laki
nne za sukari itakayouzwa hapa nchini huku Tanzania
ikitarajia kuzalisha spiriti na hamira
itakayouzwa nchini Oman pamoja na nchi za Mashariki ya kati.
‘’ Wafanyabishara wetu na wale wa Oman
kupitia makubaliano haya watanufaika na fursa za uwekezaji kwa kupata mikopo
mbalimbali na tayari mtaji wa Dola za Marekani milioni 25
zitatumika kwa wawekezaji hao’’ Amesema Bibi. Kasiga.
Aidha,amesema Wafanyabiashara kutoka
Oman tayari wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo madini,
viwanda na biashara, kilimo, utalii pamoja na ujenzi wa
nyumba za kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Ameongeza kuwa uwekezaji utaongeza ajira
akitoa mfano wa kiwanda cha Sukari cha Kagera
kitakachozalisha ajira 500 pamoja na kuongeza wigo wa soko.
Katika hatua amesema
kuwa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa itawapeleka watumishi 105 wa ngazi mbalimbali katika Balozi 35 zilizo
katika nchi mbalimbali duniani na kuwarudisha nyumbani
watumishi 79.
Bibi Mindi, ametaja sababu za kurudishwa kwa
watumishi hao kuwa ni pamoja kuisha kwa muda wao wa kuhudumu nje ya nchi ambao
ni miaka minne(tour on duty) pamoja, kustaafu na sababu mbalimbali.
Amezitaja Kada za watumishi wanaorudishwa
nchini kuwa ni mabalozi, wahasibu, makatibu muhktasi na maofisa wa ngazi
mbalimbali.
Hata hivyo, hadi kufikia
sasa tayari mabalozi watatu wamerudishwa nchini ambao ni Balozi Peter Kalaghe
aliyekuwa Uingereza, Balozi James Msekela aliyekuwa Italia na Balozi Batilda
Burian aliyekuwa Japan kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa
Januari 25, 2016 kuitaka wizara hiyo kuwarudisha nchini mabalozi waliomaliza
muda wao wa kuhudumu ili wapangiwe kazi nyingine.
Post a Comment