KONGAMANO KUBWA LA KIBIASHARA KUFANYIKA KIGALI
Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabariblog
Kongamano kubwa la biashara kati ya
Tanzania na Rwanda limepangwa kufanyika Mei 20 mwaka huu katika ukumbi wa
Serena Hotel ulioko Jijini Kigali Rwanda.
Kongamano hilo limetangazwa rasmi
leo na Makamu Mwenyekiti wa Biashara ,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Dr.
Kingu Mtemi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu malengo ya
mkutano huo.
“Kongamano hili lina lengo la
kukuza biashara, uwekezaji pamoja na kuongeza ushirikiano baina ya
wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda, ni fursa kubwa sana itakayosaidia kukuza
uchumi wa nchi yetu” alisema Dr. Mtemi.
Dr. Mtemi ameongeza kuwa kongamano
hili sio ya kukutana na kujadili changamoto na fursa za kibiashara tu bali
itashirikisha wafanyabiashara wanaotaka kuonyesha bidhaa zao katika nchi ya
Rwanda.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama
cha Wamiliki wa Malori na Usafirishaji (TATOA), Bw. Emanuel Kakuyu amesema kuwa
hii ni fursa nzuri kwa Tanzania kwa sababu Rwanda inapitisha asilimia 80 ya
bidhaa zake kwenye bandari ya Dar es Salaam,Tanzania na asilimia 90 ya bidhaa
hizo zinasafirishwa na malori kwenda Rwanda kwa hiyo biashara kati ya Tanzania
na Rwanda ikiimarishwa,pato la Taifa litaongezeka.
Aidha, Afisa Miradi wa Biashara,
Hurbert Kissasi amewataja waandaji wa Kongamano hilo kuwa ni: Chama cha
Wafanyabiashara , Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Mamlaka ya Maendeleo na
Biashara Tanzania (TANTRADE),Chama cha Wamiliki Malori Tanzania (TATOA), 361 Degrees
pamoja na Shirikisho la Sekta Binafsi Rwanda (PSF).
Rai hii ya kushirikiana kibiashara
kati ya Tanzania na Rwanda ilitolewa Machi 6 mwaka huu na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais Paul
Kagame wa Rwanda walipokuwa wanazindua daraja la Rusumo na kituo cha pamoja cha
kibiashara kilichopo mpakani mwa Rwanda na Tanzania.
Kwa kipindi cha miongo kadhaa
Rwanda imekuwa mshirika mkubwa wa Tanzania kibiashara katika Ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati. Hivyo Kongamano hili litakuza ushirikiano huu na kuleta tija
kwa pande zote mbili ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Post a Comment