Wizara ya Afya yatoa tahadhari ya homa ya manjano

Na
Jacquiline Mrisho
mwambawahabariblog
Wizara
ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari juu ya
ugonjwa wa homa ya manjano ambao umethibitika kuwepo nchi ya jirani ya Kenya.
Tahadhari
hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokua akiongea na waandishi wa habari kuhusu
mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu nchini ambapo katika wiki ya tarehe 14
Machi hadi 20 Machi mwaka huu takwimu zinaonyesha kuwa kati ya Mikoa 13 yenye
wagonjwa wa kipindupindu , jumla ya wagonjwa 738 na vifo
16 vimeripotiwa huku Mkoa wa Manyara ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa
wengi wa kipindupindu.
Akielezea
kuhusu ugonjwa wa homa ya manjano,Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa ugonjwa huu
unasababishwa na virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes na baadhi ya
dalili zake ni homa, kuumwa kichwa,maumivu ya misuli na mgongo,kupoteza hamu ya
kula pia kutoka damu sehemu za mwili zilizo wazi.
“Wizara
inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa wa homa ya manjano kwa wananchi wote na hasa
wanaokaa mipakani mwa nchi ya Kenya kwa kuwa ugonjwa huu hauna tiba kamili ila
una chanjo, mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zinazojitokeza ikiwa ni pamoja
na kupewa dawa za kushusha homa, maumivu, kuongezewa maji mwilini kwa kunywa au
kuwekewa dripu”alisema Waziri Ummy.
Aidha,
Waziri Ummy amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kupambana
na magonjwa ya kuambukiza kwa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa
wagonjwa na utaratibu wa utoaji taarifa za magonjwa ya kuambukiza, kuhakikisha wasafiri
wanaoingia na kutoka nchi zenye hatari ya ugonjwa huo wanapewa chanjo kabla ya
kuingia nchi nyingine, kutoa elimu ya afya kwa wananchi, kuandaa timu za
wataalam, vifaa tiba na chanjo za kutosha ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo
endapo utajitokeza nchini kwa kusimamia na kuhimiza usafi wa mazingira na
kuzingatia kanuni za afya.
Pia,amewaonya
maofisa wanaotoa chanjo ya homa ya manjano walioko katika vituo vya Afya vya
kupokelea wageni wanaoingia na kutoka nchini kuacha mtindo wa kupokea rushwa na
kuwapitisha watu bila kupatiwa chanjo.
Mwisho,
ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kushirikiana kwa karibu na
wataalamu wa afya walioko katika maeneo yao kwa kutoa taarifa haraka
kwenye uongozi husika endapo kuna mgonjwa mwenye dalili za kipindupindu au homa
ya manjano.
Post a Comment