WAFANYAKAZI zaidi ya 360 wa kiwanda cha saruji cha Dangote
mkoani Mtwara, wamekamatwa kwa kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali vya
Uhamiaji.
Kamatakamata hiyo imekuja baada ya agizo la Waziri wa Mambo ya
Ndani, Charles Kitwanga la kuwakamata wahamiaji haramu na wageni wanaofanya
kazi bila vibali.
Jana, ofisi ya Uhamiaji ya mkoa ilifanya operesheni katika
kiwanda hicho, lakini haikupewa ushirikiano na uongozi.
Ofisa Uhamiaji wa mkoa, Zakayo Mchele alisema walifika kiwandani
hapo kufanya ukaguzi, lakini walikosa ushirikiano kutoka kwa Meneja Mkuu
aliyefahamika kwa jina la Vidya Digixt.
Mchele alisema kutokana na meneja huyo kutotoa ushirikiano,
wanamshikilia ili kusaidiana na Uhamiaji kuwabaini wafanyakazi wanaoishi bila
uhalali na pia watamfikisha mahakamani.
Alisema licha ya kukosa ushirikiano, wafanyakazi 117 wa kiwanda
hicho walipeleka maombi ya kutaka kupewa vibali vya kazi.
Mchele alisema walifanya msako katika mpaka wa Kilambo na Wilaya
ya Tandahimba na kuwakamata watu 48 raia wa Ethiopia ambao walisafirishwa kwa
malori kutoka Kenya.
“ Pia, tuliwakamata raia wengine wawili wa Msumbiji wakiwa na
kadi za kupigia kura (za Tanzania) na kukamatwa siyo kwamba msako ulikuwa
haufanyiki siku za nyuma,” alisema.
Alisema mwaka jana idadi ya watu walioingia nchini bila kibali
kwa Mkoa wa Mtwara walikuwa 121.
Afisa huyo alisema katika operesheni hiyo kesi zilizopelekwa
mahakamani ni 36 ambazo zilikamilika na wahusika kutiwa hatiani na kutozwa
faini, huku wengine wakipewa adhabu ya kutumikia kifungo.
credit mpekuzi
Post a Comment