SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA BARUA PEPE ZA KAWAIDA KATIKA MAWASILIANO YAKE.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto) kuhusu utendaji wa Wakala hiyo leo
wakati wa ziara ya kikazi
ya Mhe. Angella Kairuki katika Ofisi za Wakala hiyo leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa
mwambawahabari.blogspot.com
Serikali imepiga marufuku
matumizi ya Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea
taarifa za Serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo
rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali
kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia ya Mtandao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe.Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa
Wakala ya Serikali Mtandao ( e Government Agency) wakati wa ziara yake ya
kukagua utendaji na ufanisi wa matumizi ya TEHAMA Serikalini.
“Sasa kuna
watumishi 7000 wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali ,idadi hii ni ndogo
lazima iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali
kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza
na kuongeza kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye
mawasiliano binafsi.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa
uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya
TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao
mbalimbali ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua
Pepe za Serikali.
Mhe. Kairuki amewataka watendaji
wa Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili
kuhakikisha kuwa Wizara, Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa na mfumo
rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano.
“Katika
hili ninatoa siku 60 muhakikishe kuwa mnakamilisha kwa Taasisi zilizobaki ili
kwa wale watakaopuuzia hatua zianze kuchukuliwa” Ameeleza Mhe. Angella.
Aidha, ametoa wito kwa watendaji
wa Wakala hiyo kuweka mpango wa
kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo kazini kwa kujenga utaratibu wa kuwarithisha
uzoefu watumishi ili kuendelea kuimarisha ufanisi na utendaji wa Wakala hiyo.
Mhe. Kairuki amewataka kuwa
wabunifu katika kuanzisha mifumo mipya ya TEHAMA ili kuimarisha dhana ya Serikali
mtandao ili kupunguza
gharama hadi kufikia asilimia 5 ya fedha zinazotumika kuendeshea masuala
mbalimbali ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA.
Akizungumzia kuhusu ununuzi wa
vifaa vya TEHAMA serikalini ameitaka Wakala hiyo kutoa ushauri ili kudhibiti
mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya
fedha katika kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa wakati vinaweza kupatikana
kwa bei ya kawaida.
“katika
hili Serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika katika upotevu wa
mapato muhakikise mnazisaidia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika
masuala ya ununuzi wa mifumo na vifaa vya TEHAMA ili mifumo inayonunuliwa iwe
na manufaa kwa wananchi na thamani halisi ya fedha”
Amesema Serikali itaendelea
kuboresha utoaji wa huduma kupitia mtandao ili wananchi waweze kupata huduma
hizo mahali walipo kwa
gharama nafuu na kutoa wito kwa watumishi wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov) kuwa wabunifu katika kutengeneza
programu mbalimbali na mifumo salama itakayowasaidia wananchi kupata huduma.
Aidha, katika hatua nyingine
ameitaka e-Gov kuendelelea kujenga uwezo katika kudhibiti dharura na majanga
mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika matumizi ya TEHAMA na kuitaka Wakala
hiyo iendelee kulifanyia kazi suala la kuwezesha mifumo ya Serikali kuzungumza
kati ya taasisi moja hadi nyingine ili huduma zote ziweze kupatikana katika eneo
moja na kuondoa urudufu wa
mifumo iliyopo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
Wakala ya Serikali Mtandao (e-Gov) Dkt. Jabiri Bakari akitoa taarifa ya
utendaji wa Wakala hiyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto
mbalimbali toka kuanzishwa kwake Julai 11, 2012 imeendelea kupata ufanisi
katika uimarishaji wa Serikali Mtandao.
Amesema kuwa Wakala hiyo
inaendelea kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinawafikia wananchi kupitia
mtandao mahali walipo na kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo la huduma zote za
Serikali kupatikana chini ya dirisha moja.
Aidha amesema kuwa Wakala ya
Serikali Mtandao itaendelea kuhakikisha kuwa usimamizi wa viwango vya matumizi
ya TEHAMA katika Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali vinazingatiwa.
Post a Comment