Ads

NHIF KUBORESHA HUDUMA ZAKE MWAKA 2016

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Michael Mhando akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es salaam kushoto ni  Mkurugenzi wa Masoko, Elimu kwa Umma na Utafiti Rehani Athumani (picha na Jacquiline  Mrisho)

Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabari.blogspot.com

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unategemea kuboresha baadhi ya huduma zao ifikapo 2016 ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hizo
kwa wananchi.

Akiyasema hayo leo Jijini Dar es salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu Michael Mhando amezitaja baadhi ya huduma ambazo wana mpango wa kuziboresha kwa mwaka 2016  zikiwemo za kuongeza huduma ya matibabu ya moyo kwa kutumia bima ya NHIF,kutoa mikopo ya dawa,kurekebisha mfumo wa ulipaji wa baadhi ya huduma pia kubadili gharama za huduma ambazo zinalipwa kwa watoa huduma ili kuendana na hali halisi ya mfumuko wa bei.

‘’mimi binafsi nimefurahishwa na agizo la Mheshimiwa Rais  kutengeneza maduka ya dawa kila Hospitali ya Mkoa na nitakua tayari kushirikiana nao kwa kuwakopesha fedha kwa ajili ya kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi’’alisema  Mhando.

Naye Mkurugenzi wa Masoko, Elimu kwa Umma na Utafiti Rehani Athumani amezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili zikiwemo za kukosekana kwa dawa katika hospitali husika pamoja na tabia ya baadhi ya wanachama kugushi baadhi ya nyaraka wakati wa usajili.

Aidha,Bw. Rehani Athumani ametaja hatua itakayochukuliwa ili kudhibiti ubora wa huduma zitolewazo na mfuko huo kuwa ni kufanya ukaguzi wa kushtukiza ujulikanao kwa jina la kitaalamu kama ‘Medical surveillance’ katika vituo vya matibabu ili kuona ubora wa huduma wanazotoa kwa wananchi.

Katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya utahakikisha  kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watoa huduma ambao wataongeza bei za huduma kwa wanachama wa mfuko huo na maboresho hayo  hayataathiri kiwango cha michango kinachotolewa na wanachama.

No comments