Ads

TAEC Yajipanga Kuimarisha Udhibiti na Usalama wa Teknolojia ya Nyuklia Nchini





Na.John Luhende 

Mwamba wa habari 

Dar es salaam 

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imeeleza dhamira yake ya kuimarisha uwezo wa kusimamia na kudhibiti teknolojia ya nyuklia nchini, hususan katika maandalizi ya mpango wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia.


Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa shughuli zote zinazohusiana na teknolojia hiyo zinatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama na ulinzi (Safety and Security), sambamba na kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa TAEC kukabiliana na kasi ya maendeleo ya sekta ya nyuklia nchini.


Akizungumza katika warsha ya mafunzo na maandalizi ya tathmini ya miundombinu ya nyuklia, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi wa TAEC, Remigius Ambrosi Kawala, amesema warsha hiyo inalenga kuwawezesha wadau kufanya tathmini ya hatua ambazo Tanzania imefikia katika maeneo 19 ya miundombinu ya nyuklia, pamoja na kujiandaa kwa tathmini ya kimataifa inayojulikana kama Integrated Nuclear Infrastructure Review (INIR).


Amesema tathmini hiyo ni muhimu kwa kuonesha hatua ambazo nchi imepiga, ilipo kwa sasa na maeneo inayopaswa kuyaboresha ili kufikia malengo yake ya kuendeleza teknolojia ya nyuklia.


Kawala amesema TAEC imekuwa ikishiriki katika maandalizi hayo tangu hatua za awali, ikijikita katika kuhakikisha masuala ya usalama na ulinzi wa teknolojia ya nyuklia yanazingatiwa katika kila hatua ya utekelezaji wa mpango huo.


Ameongeza kuwa mkakati mwingine muhimu ni kuijengea TAEC uwezo wa kitaalamu, kitaasisi na kiutendaji ili iweze kutekeleza ipasavyo majukumu yake ya udhibiti kadiri Tanzania inavyopiga hatua kuelekea katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia.


Aidha, amesema warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wadhibiti, kwa lengo la kubainisha majukumu na mchango wa TAEC katika maendeleo ya sekta hiyo na namna bora ya kuyatekeleza.


Amebainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo ni kuhakikisha shughuli za udhibiti wa teknolojia ya nyuklia zinatenganishwa na shughuli za uendelezaji wa teknolojia hiyo, ili kuweka mfumo imara unaozuia migongano ya majukumu na kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa kuzalisha umeme wa nyuklia unafanyika kwa ufanisi bila vikwazo vya kiutendaji hapo baadaye.


Amesisitiza kuwa utenganishaji huo ni muhimu katika kuhakikisha mfumo wa udhibiti unakuwa huru na madhubuti, huku maendeleo ya teknolojia ya nyuklia nchini yakiendelea kwa kuzingatia usalama na viwango vinavyokubalika kimataifa

No comments