MASAFA YA REDIO FM NI RASILIMALI ADIMU, WADAU WASHAURIWA KUTUMIA MAJUKWAA YA MTANDAONI
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeripotiwa kukosa masafa ya kuanzisha kituo chake cha redio kupitia mfumo wa FM kutokana na ufinyu wa masafa yaliyopo, hali iliyokifanya chuo hicho kushauriwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha redio ya mtandaoni (Online Radio), kama njia mbadala ya kuwafikia wasikilizaji.
Akifafanua kuhusu changamoto hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Albert Richard, amesema masafa ya redio ni rasilimali adimu ambayo haiwezi kuzalishwa upya, hivyo matumizi yake yanahitaji kusimamiwa kwa umakini kutokana na ufinyu wa rasilimali hiyo.
Richard amesema masafa ni rasilimali inayofanana na viwanja vya ardhi, ambavyo havizalishwi tena, hivyo kadri vinavyotumika ndivyo nafasi ya kupata maeneo mapya inavyopungua.
Amesema Tanzania ina eneo la takribani kilomita za mraba 954,000, ambalo ni rasilimali ya kipekee isiyoweza kuongezwa, na hali hiyo inafanana na masafa ya mawasiliano ambayo yana ukomo.
Ameeleza kuwa katika utangazaji wa redio za FM, masafa huanzia 87.5 MHz hadi 108 MHz, sawa na wigo wa takribani MHz 20.5. Kila kituo cha redio kinahitaji mgao wa takribani MHz 0.8 ili kiweze kufanya kazi.
Richard amesema mawimbi ya redio za FM yanaweza kufikia umbali wa kilomita 50 hadi 70, hali inayofanya upatikanaji wa masafa mapya kuwa changamoto zaidi katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Tanga na Arusha, ambako masafa mengi tayari yameshagawiwa kwa vituo mbalimbali vya redio.
Amesisitiza kuwa kutokana na hali hiyo, waombaji wapya hawawezi kupewa masafa ambayo tayari yametumika na kugawiwa kwa vituo vingine, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuangalia njia mbadala za kufikisha huduma za utangazaji kwa wananchi.
Kutokana na changamoto hiyo, UDOM imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha redio ya mtandaoni badala ya kusubiri upatikanaji wa masafa ya FM. Hatua hiyo inaelezwa kuwa njia mbadala ya kuwezesha chuo hicho kuendelea na shughuli za utangazaji, kutoa taarifa kwa jamii, kuelimisha na kuwafikia wasikilizaji kupitia majukwaa ya kidijitali.
Richard amewashauri pia wadau wa utangazaji na wanaotaka kuanzisha vituo vya redio kuangalia fursa zilizopo katika majukwaa ya mtandaoni, ambayo yanatoa nafasi pana zaidi ya kusambaza maudhui bila kukabiliwa na ukomo wa masafa ya FM kwa namna hiyo hiyo.




Post a Comment