Ads

TBS Yaimarisha Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa Nchini

 



Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limepima sampuli zaidi ya 188,952 na kukagua shehena za bidhaa 610,028 zilizoingizwa nchini katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, kwa lengo la kulinda afya na usalama wa watumiaji.


Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, alisema Serikali imetumia Sh bilioni 12.9 kununua mashine za kisasa za maabara, huku maabara zote 14 za shirika hilo zikipata ithibati za umahiri wa kimataifa.


Alieleza kuwa TBS pia imeandaa viwango 3,901, kutoa vyeti na leseni za ubora 3,940 kwa wazalishaji, kusajili bidhaa 9,731 za chakula na vipodozi, pamoja na kukagua magari 249,386 yaliyotumika kabla ya kuingizwa nchini.


Aidha, shirika hilo linaendelea na miradi ya ujenzi wa maabara na ofisi za Viwango House Dodoma na Mwanza, huku likitoa mafunzo kwa wadau 6,824 kuhusu viwango na udhibiti wa ubora.

 Hatua hizo zinalenga kukuza uzalishaji wa bidhaa bora, kuimarisha biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.


No comments