Ads

NeST Kuimarisha Uwazi na Ufanisi katika Ununuzi wa Umma




Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba, asema mfumo wa kielektroniki wa NeST warahisisha michakato ya ununuzi na kuimarisha uwajibikaji


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Denis Simba, amesisitiza umuhimu wa Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa michakato ya ununuzi wa umma nchini.


Simba amesema mfumo huo, ulioanza kutumika rasmi Septemba 2023, umewekwa ili kurahisisha michakato ya ununuzi wa umma kwa njia ya kielektroniki, kupunguza matumizi ya nyaraka za karatasi na kuwezesha usimamizi wa shughuli za ununuzi kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.


Ameeleza kuwa NeST ina moduli kuu sita zinazohusisha usajili wa kielektroniki, uendeshaji wa zabuni, malipo, usimamizi wa mikataba, katalogi ya bidhaa na huduma, pamoja na mnada wa kielektroniki wa kushusha bei. Moduli hizo zinawezesha kushughulikia hatua mbalimbali za mchakato wa ununuzi kupitia mfumo mmoja wa kielektroniki.


Aidha, Simba amesema NeST imeunganishwa na mifumo mingine zaidi ya 30, ikiwemo ya taasisi za kibenki, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mfumo wa TAUSI na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Ushirikishwaji huo wa mifumo unalenga kurahisisha upatikanaji na uhakiki wa taarifa, kupunguza urudufu wa nyaraka na kusaidia kuimarisha uadilifu katika michakato ya ununuzi wa umma.


Amebainisha kuwa umuhimu wa mifumo hiyo unaenda sambamba na jukumu la PPRA la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2024, kwa kuhakikisha taratibu za ununuzi zinafuatwa na thamani halisi ya fedha za umma inapatikana.


Akizungumzia ukubwa wa sekta hiyo, Simba amesema takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika kupitia ununuzi wa umma, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuwa na mifumo inayosaidia kusimamia matumizi ya fedha hizo kwa uwazi na ufanisi.


Kwa mantiki hiyo, matumizi ya NeST ni sehemu muhimu ya jitihada za kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma, kuimarisha ushindani na uwajibikaji, pamoja na kurahisisha ushiriki wa wadau katika fursa za zabuni za Serikali.

No comments