Ads

Waziri Kairuki aitaka TTCL kuongeza wigo wa huduma na kuboresha huduma kwa wateja

 

DAR ES SALAAM:

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, ameitaka Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza wigo wa huduma, idadi ya wateja na kuboresha ubora wa huduma za mawasiliano ili kuongeza tija ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Mkongo wa Taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi  wa Program ya Faiba mlangoni kwako, Waziri Kairuki alisema TTCL imepewa dhamana ya kuusimamia na kuumiliki Mkongo wa Taifa, hivyo inapaswa kuhakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa kwa kampuni na Taifa kwa ujumla.

Amesema TTCL inapaswa kuendelea kuweka malengo makubwa na kuwahamasisha watumishi wake kufanya kazi kwa mtazamo wa kibiashara ili kutimiza matarajio yaliyowekwa.

Waziri Kairuki alitoa maelekezo kadhaa kwa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na watumishi wa TTCL, akianza kwa kuitaka kampuni hiyo kupanua wigo wa huduma na kuongeza idadi ya wateja.

Amesema huduma za Mkongo wa Taifa na intaneti hazipaswi kuishia katika maeneo machache pekee, bali zinapaswa kufikishwa katika makazi yanayokua, vituo vya biashara, masoko, maeneo ya viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

“Mtandao usipanuke kwa kilomita pekee; upanuke pia kwa idadi ya wananchi wanaotumia mtandao,” alisema.

Aidha, aliiitaka TTCL kuwa na mpango mahsusi wa kubadilisha home passes kuwa wateja hai, ili uwekezaji unaofanywa katika miundombinu uweze kuleta mapato na kuongeza tija kwa kampuni.

Katika kuboresha upatikanaji wa huduma, Waziri Kairuki alisisitiza umuhimu wa kurahisisha taratibu za usajili na kupunguza muda wa kuunganisha huduma. Alisema TTCL inapaswa kushirikiana na serikali za mitaa, waendelezaji wa makazi, wamiliki wa majengo na jumuiya za wafanyabiashara ili kurahisisha upanuzi wa huduma.

Kuhusu ubora wa huduma, Waziri Kairuki alisema mteja anayelipia huduma ya intaneti ya fiber anatarajia kupata kasi iliyoahidiwa pamoja na huduma yenye uhakika.

Aliitaka TTCL kuimarisha ufuatiliaji wa mtandao, kufanya matengenezo ya kinga na kuhakikisha huduma zinaporejea baada ya kutokea hitilafu zinarejeshwa kwa haraka.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuboresha huduma kwa wateja, akisema mteja anapaswa kusikilizwa, kuheshimiwa na kushughulikiwa kwa wakati anapowasilisha changamoto.

“TTCL ndiyo imfuatilie mteja, TTCL ndiyo imjulishe hatua zilizofikiwa na TTCL ndiyo ihakikishe suluhisho la changamoto au tatizo la mteja limepatikana,” alisema.

Ameitaka kampuni hiyo kuweka njia rahisi za mawasiliano na wateja, pamoja na mfumo madhubuti wa kufuatilia malalamiko na kuhakikisha yanashughulikiwa ndani ya muda uliowekwa kwa mujibu wa Client Service Charter.

Waziri Kairuki amesema huduma bora kwa wateja ni msingi wa kujenga uaminifu na ni nguzo muhimu ya ukuaji wa TTCL.

Katika hatua nyingine, aliitaka TTCL kuhakikisha huduma zake zinapatikana kwa gharama nafuu na kubuni vifurushi vinavyoendana na uwezo wa kaya, familia na makundi mbalimbali ya wananchi.

Ametaja wanafunzi, vijana, wafanyakazi wa majumbani na mashambani, wavuvi, wachimbaji wa migodi, wafanyabiashara wadogo na wa kati, pamoja na taasisi, kuwa miongoni mwa makundi yanayopaswa kuzingatiwa katika upangaji wa gharama za huduma.

Amesema gharama za kuunganishwa, vifaa na vifurushi hazipaswi kuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma za mawasiliano. Aidha, bei zinapaswa kuwa wazi, rahisi kueleweka na kuendana na ubora wa huduma inayotolewa.

“TTCL tunapaswa kujiendesha kibiashara, lakini unafuu na uendelevu si malengo yanayopingana. Kwa kadri shirika linavyoongeza wateja, kuboresha ufanisi na kudhibiti gharama, ndivyo tutakavyoweza kutoa huduma nafuu na wakati huo huo kukuza mapato ya shirika,” alisema.

Waziri Kairuki pia amesisitiza umuhimu wa TTCL kusimamia miradi yake kwa uwajibikaji na nidhamu ya kibiashara. Aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha wakandarasi na wazabuni wanasimamiwa ipasavyo ili kazi zikamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia masharti ya mikataba.

Amesema kila shilingi inayowekezwa au kutumika na kampuni inapaswa kuleta thamani kwa TTCL na Taifa.

Aidha, alitaka taarifa za utekelezaji wa miradi zisijikite katika idadi ya home passes pekee, bali zizingatie pia idadi ya wateja hai waliounganishwa, muda wa kuunganisha huduma, upatikanaji wa mtandao, kasi halisi ya huduma, muda wa kutatua malalamiko na kiwango cha kuridhika kwa wateja.

Amesema vipimo hivyo vinapaswa pia kuhusisha ufanisi wa huduma, unafuu wa vifurushi na mapato yanayotokana na uwekezaji.

“Tunachokipima ndicho ambacho tunaweza kukiboresha,” alisisitiza.

Mwisho, Waziri Kairuki aliipongeza TTCL kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kuboresha huduma zake, huku akisisitiza kuwa kampuni hiyo inapaswa kuongeza juhudi zaidi ili kutimiza matarajio makubwa yaliyowekwa na Serikali.

No comments