DSE na NBC waunganisha mifumo kuwawezesha Watanzania kuwekeza kupitia simu Dar es Salaam
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kwa kushirikiana na Benki ya NBC Tanzania, limezindua huduma ya kuunganisha mifumo ya DSE Hisa Kiganjani na NBC Kiganjani, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji na dhamana kwa wananchi kupitia simu zao za mkononi.
Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za DSE zilizopo Morocco Square Exchange Tower, Dar es Salaam, ambapo viongozi kutoka DSE, NBC na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) walieleza umuhimu wa teknolojia hiyo katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtaraji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Peter Nalitolela alisema ushirikiano huo umeleta fursa kwa wateja wa NBC kupata huduma za uwekezaji moja kwa moja kupitia mfumo wa NBC Kiganjani.
Alisema mteja wa NBC anapoingia kwenye huduma ya NBC Kiganjani ataweza kuona alama ya DSE, na kwa kubofya ataelekezwa kwenye huduma inayomwezesha kushiriki katika uwekezaji katika soko la hisa.
“Tunataka kuwaondoa Watanzania kwenye mtazamo wa zamani kwamba akaunti ya benki ni kwa ajili ya kuweka akiba pekee. Ni wakati wa kutoka kwenye kuweka fedha tu na kuanza pia kuwekeza,” alisema Nalitorela.
Aliongeza kuwa hata mtu ambaye bado si mteja wa NBC anaweza kupakua programu ya NBC Kiganjani kupitia Play Store au App Store, kisha kufungua akaunti kwa kutumia namba yake ya NIDA na kufuata hatua zinazoelekezwa.
Kwa upande mwingine, alisema wananchi ambao hawajaanza kuwekeza katika DSE wanaweza kuanza safari yao ya uwekezaji kupitia DSE Hisa Kiganjani kwa kupakua programu hiyo na kufuata taratibu za usajili.
Kwa mujibu wa Nalitolela, huduma hizo zinamwezesha mwananchi kufanya shughuli mbalimbali za kifedha kwa njia ya kidijitali wakati wowote na mahali popote, ikiwamo kulipa bili za huduma kama umeme na maji, pamoja na kufanya uwekezaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa CMSA, Alfred Mkombo, alisema kuunganishwa kwa mifumo ya NBC Kiganjani na DSE Hisa Kiganjani ni hatua muhimu katika kufikisha huduma za masoko ya mitaji na dhamana kwa wananchi wengi zaidi.
Alisema wateja wa NBC sasa wanaweza kufikia huduma za DSE kupitia simu zao na kuwekeza katika dhamana zilizoorodheshwa katika soko hilo bila kulazimika kufika katika ofisi za soko.
“Ni nafasi nzuri ya kuwafikishia wananchi wengi zaidi huduma za masoko ya mitaji na kuwawezesha kupata fursa za kuwekeza na kunufaika na masoko ya mitaji,” alisema Mkombo.
Aidha, alizitaka taasisi zinazohusika kuhakikisha wananchi wanapata elimu na msaada wa kutosha katika kutumia mifumo hiyo, hasa wale ambao bado hawajazoea huduma za kidijitali.
Alisema ni muhimu kuweka watumishi watakaowaongoza wananchi hatua kwa hatua katika kutumia mifumo hiyo ili waweze kuifahamu na kuitumia kwa ufanisi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema benki hiyo inafurahia ushirikiano huo unaowawezesha wateja wake kushiriki katika uwekezaji katika Soko la Hisa la Dar es Salaam moja kwa moja kupitia akaunti zao za NBC Kiganjani.
Alisema hata wananchi ambao bado si wateja wa NBC wanaweza kufungua akaunti kupitia NBC Kiganjani kwa kutumia namba yao ya NIDA na namba ya simu, huku mchakato wa kufungua akaunti ukichukua muda mfupi.
Alisisitiza kuwa NBC inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha mifumo yake ya kidijitali inakuwa salama na kuwaalika Watanzania kutumia fursa hiyo kuanza safari ya uwekezaji.
Uunganishwaji wa mifumo hiyo unatarajiwa kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji, kuongeza idadi ya Watanzania wanaoshiriki katika uwekezaji na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika huduma za kifedha.
Wananchi wanahimizwa kutumia huduma za NBC Kiganjani na DSE Hisa Kiganjani kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji na kuanza kushiriki katika soko la mitaji kwa kufuata taratibu na masharti yaliyowekwa.


Post a Comment