Ads

NHC YATAKIWA KUFANYA UTAFITI WA UJENZI WA NYUMBA BORA NA NAFUU.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati yeye na Naibu wake Kaspar Mmuya walipotembelea shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari 2026. Katikati ni Naibu Waziri Kaspar Mmuya na kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa Bw, Hamad Abdallah.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya  akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati yeye na Waziri wa Ardhi  walipotembelea shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari 2026.

Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Bw. Hamad Abdallah akizungumza jambo katika kikao cha watumishi wa NHC na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Kaspar Mmuya.



Sehemu ya watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakiwa katika kikao cha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Naibu wake kilichofanyika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari 2026.

...........

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufanya tafiti za kina zitakazowezesha ujenzi wa nyumba bora na zenye gharama nafuu ili wananchi wa kipato cha chini wanufaike na miradi ya shirika hilo.

Dkt. Akwilapo ametoa kauli hiyo leo tarehe 5 Januari, 2026, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na watumishi wa NHC wakati wa ziara yake ya siku moja ya kulifahamu shirika hilo, akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya.

“Mfanye tafiti za jinsi ya kujenga makazi bora kwa gharama nafuu, na muelewe unafuu huo unamlenga nani, kwa kuwa kuna makundi mbalimbali ya Watanzania,” amesema Dkt. Akwilapo.

Aidha, amelitaka shirika hilo kufanya tafiti kuhusu upatikanaji wa teknolojia za kisasa zitakazosaidia kujenga nyumba bora na za gharama nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Watanzania wengi wanalitazama Shirika la Nyumba la Taifa kama suluhisho la changamoto wanazokumbana nazo katika ujenzi wa nyumba, kuanzia ununuzi wa vifaa vya ujenzi hadi upatikanaji wa mafundi wenye ujuzi, hivyo NHC inapaswa kuwa kimbilio la uhakika.

Ameeleza kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanasisitiza umuhimu wa wananchi kupata makazi bora, salama na yenye huduma muhimu kama umeme na maji. Hivyo, amewataka watumishi wa NHC kulifanya suala la makazi bora kuwa kipaumbele, hasa ikizingatiwa ongezeko la watu mijini linalochochea mahitaji makubwa ya nyumba.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amepongeza mabadiliko ya kimfumo yanayoendelea kufanyika ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa, huku akiwahimiza watumishi wa NHC kujipanga kumiliki nyumba.

“Nitashangaa kuona mtumishi wa NHC hana nyumba. Mjipange kumiliki nyumba, na uongozi uone fahari kwa kuwawezesha watumishi wake kumiliki makazi. Mafanikio ya sekta ya ardhi yaonekane kwa vitendo,” amesema Mhe. Mmuya.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amewasilisha taarifa ya mipango, mikakati na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya shirika hilo, na kumhakikishia Waziri kuwa NHC itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuzingatia sera na miongozo ya Serikali.

Bw. Hamad amesema kwa sasa NHC inatekeleza miradi 67 yenye thamani ya shilingi bilioni 458.2, ambapo miradi 60 tayari imekamilika na miradi 7 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Baadhi ya miradi iliyokamilika ni pamoja na majengo 8 ya Ofisi za Wizara katika eneo la Mtumba, Dodoma, Soko la Madini ya Tanzanite Mererani, Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete, Ghala la Chakula Masasi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, pamoja na Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

No comments