Ads

ETDCO YAKAMILISHA MRADI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME KILOVOLTI 132 IPOLE - INYONGA

Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekamilisha ujenzi wa laini mpya ya umeme ya kilovolti 132 kutoka Ipole, Wilaya ya Sikonge, Tabora hadi Inyonga Wilaya ya Mlele  Mkoa wa Katavi.

Laini hiyo yenye urefu wa kilomita 133 iliyowashwa, ni hatua muhimu ya kuunganisha Mkoa wa Katavi katika  Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza.

Akizungumza wakati wa kuwasha laini hiyo katika kituo cha kupoza umeme cha Inyonga Mkoani Katavi, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, CPA Sadock Mugendi, amesema ujenzi umekamilika kwa asilimia 100, huku  akiishukuru serikali na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kuiamini kampuni hiyo kutekeleza mradi huo wa kimkakati.

Mhandisi wa Mradi kutoka TANESCO, Mhandisi Dalali Lunyamila, amesema kituo cha Inyonga kina uwezo wa kupokea Megawatts 12, ambapo  mahitaji ya sasa ya Wilaya ya Mlele ni Megawatts 4, na hivyo kufanya uwepo na ziada ya Megawatts 8 ya matumizi ya sasa na baadaye.

Mhandisi Lunyamila amesema kuwa  wananchi wa Wilaya ya Mlele na  Majimoto wanatarajiwa kupata huduma ya umeme wa uhakika kupitia gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza na kusaidia  kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Dismas Massawe, amesema kuwa laini hiyo itakuwa kwenye kipindi cha matazamio kwa saa 48 kabla ya kuanza kutumika rasmi.

Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupeleka umeme wa uwakika wa grid kwenye maneneo ambayo  yalikuwa hayajaonganishwa na grid kama vile Katavi kwa lengo la  kuchochea maendeleo kwa kutumia Nishati safi, salama, na rafiki kwa mazingira.





No comments