Historia Yaandikwa: Bilioni 4.6 Kuendeleza Bunifu za Watanzania
Katika hafla hiyo, Prof. Mkenda aliwapongeza CRDB Foundation kwa ujasiri wao wa kuwekeza kwa wabunifu wa Kitanzania, akisema huo ni mfano wa taasisi binafsi zinavyoweza kuchangia maendeleo ya kitaifa. “Taasisi nyingine zijifunze kutoka CRDB Foundation. Vijana wetu hawahitaji huruma, wanahitaji fursa. Na tukiwapa fursa, watafanya maajabu,” alisema huku akiwasihi wadau wengine kujitokeza kuwekeza kwa wabunifu wa ndani.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alieleza kuwa zaidi ya wabunifu 400 kutoka mikoa mbalimbali nchini tayari wamenufaika na programu za uwezeshaji za COSTECH, na wengi wao wapo katika hatua ya kupokea mikopo. Alibainisha kuwa mikakati kama hii ni utekelezaji wa moja kwa moja wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana na kutumia maarifa, sayansi, teknolojia, na ubunifu kama suluhisho la changamoto za maendeleo.
Miongoni mwa maeneo yanayopatiwa kipaumbele ni pamoja na teknolojia za kidijitali, akili-bandia (AI), na suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii kama afya, kilimo, na elimu. Profesa Mkenda alisisitiza umuhimu wa kuingiza masomo ya akili-undi kwenye mitaala ya elimu ili kuandaa kizazi chenye uwezo wa kukabiliana na ushindani wa soko la kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Bi. Tully Esther Mwambapa, alisema kuwa taasisi hiyo imeamua kushirikiana na COSTECH kama njia ya kuendeleza miradi yenye mwelekeo wa biashara na athari kwa jamii. “Tunatambua kuwa ubunifu ni injini ya maendeleo. Kupitia uwekezaji huu, tunawaleta vijana karibu na fedha, maarifa, na mitandao ya ukuaji. Lengo letu ni kusaidia kubadilisha maisha yao na jamii kwa ujumla,” alisema Bi. Mwambapa.
Kwa ujumla, uzinduzi huu unafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya ubunifu nchini. Historia imeandikwa—wakati umefika kwa wabunifu wa Kitanzania kuinuka, kushirikiana na wadau, na kuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na maarifa. Kupitia uwekezaji huu wa bilioni 4.6, Tanzania sasa inatengeneza mazingira wezeshi kwa vijana kuandika kesho yao kupitia maarifa, teknolojia na uthubutu.
Post a Comment