Ads

SERIKALI ILIVYOJIPANGA KUWAINUA VIJANA KIUCHUMI.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na vujana jijini Dar es Salaam wakati  akifungua kongamano la siku mbili la vijana.


Baadhi ya vijana walioshiriki kongamano.

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amewataka vijana kujitambua na kujituma katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi jambo ambalo litawasaidia kufikia malengo tarajiwa.

Akizungumza leo tarehe 9, 2022 jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa kongamano la siku mbili la vijana, Mhe. Katambi amesema kuwa vijana wapaswa kuwa makini katika kuhakikisha walinda afya zao kwani ni jambo muhimu sana katika kufikia malengo yao tarajiwa.

“Ukiwa hauna afya zuri huwezi kufanya kazi kwa umakini na kujituma, hivyo tuna kila sababu ya kulinda afya zetu pamoja na kuwajibika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii” amesema Mhe. Katambi.

Amesema kuwa zipo fursa nyingi ambazo serikali wanatoka kwa vijana katika nyanja mbalimbali ikiwemo kupitia mikopo ya halmashauri, ofisi ya waziri mkuu ambapo mikopo hiyo inamgusa kila mmoja.

“Kila kijana serikali imemgusa katika elimu, ajira pamoja mikopo, tunafanya hivyo kwa sababu tunajua umuhimu wa vijana katika kuleta maendeleo kwa Taifa” amesema Mhe. Katambi.

Hata hivyo amebainisha kwa zipo baadhi ya Asasi za kiraia zinachukua fedha kutoka kwa wadhamini kwa madai zinakwenda kuwasaidia vijana jambo ambalo sio kweli.

Mhe. Katambi amesema tayari serikali imeanza mchakato wa kutathimini utendaji kazi wa Asasi zote Kiraia baada ya kubaini kuwepo kwa watu wanaozitumia kujinufaisha kiuchumi.

“Serikali haiwezi kufumbia macho suala la baadhi ya asasi zinazojitangaza kusaidia vijana wakati siyo kweli, tumeanza mchakato wa kufanya tathimini ya utendaji wa Asasi zote za kiraia zilizopo nchini kujua kama kweli wanasaidia vijana” amesema Mhe. Katambi.

Amesema kuwa kuna baadhi ni wajanja wanadai wanasaidia vijana kumbe wanajinufaisha wenyewe kujenga majumba ya kifahari kama maghorofa.

Ameeleza kuwa serikali inakuja na mipango hiyo ikiwemo kubadilisha sheria na kuipa fursa sekta binafsi kukua kwa kutambua vijana ni kundi muhimu katika kujenga uchumi wa taifa.

“Wakati jitihada za kufanya mageuzi hayo yakiendelea vijana mnatakiwa kujitokeza kwenye zoezi la kuhesabiwa  ili serikali ijue takwimu zenu na kuangalia namna ya kuboresha mahitaji yao” amesema Mhe. Katambi.

Kiongozi wa Taasisi zilizoandaa Kongamano hilo kupitia Freedom House, Bw. Daniel Lema,  amesema kuwa lengo la jukwaa hilo ni kuwaleta vijana pamoja kujadili fursa na kutengeneza mipango  na kutekeleza sera za kitaifa na kuchochea maendeleo.

“Vijana wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi ikiwemo ajira na serikali peke yake haiwezi kuwasaidia ni vizuri kuwakutanisha vijana kwenye makongamano haya kusaidia kupeana mbinu za kutumia fursa,” amesema Bw. Lema.

Bw. Ismail Biro kiongozi kutoka taasisi ya Tanzania Bora,  amesema kundi la vijana haliwezi kuepukika kwenye nyanja za kimaendeleo kwa sababu wananguvu na wanapaswa kuridhishwa kwenye mambo mengi kutokana na umuhimu wao.

Kongamano hilo linafanyika ikiwa ni katika kuelekea kilele cha siku ya kimataifa ya vijana duniani Agosti 12 Mwaka huu, ambapo vijana wametakiwa kulinda afya zao pamoja na kuwajibika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

No comments