WADAU WAKUTANA KUPINGA UKATILI SIKU YA MAADHIMISHO YA MTOTO WA AFRIKA.
Akizungumza leo tarehe 16/6/2022 jijini Dar es Salaam kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Jokate Mwegelo amesema kuwa ili kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na haki zao serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuunda mabaraza ya watoto kwenye mitaa pamoja na Kata.
Mhe. Mwegelo amesema kuwa kuunda kwa mabaraza kutasaidia kutoa fursa kwa watoto kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.
‘Walezi wahakikisha wanaimarisha ulinzi kwa watoto pamoja na kuwapatia haki zao za msingi jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha makuzi ya akili ya watoto” amesema Mhe. Mwegelo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Mwanamke na Mtoto ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Bw. Elihuruma Mabelya, amesema kuwa ni jukumu la kila mtu kuhakikisha haki za watoto zinalindwa katika jamii mbalimbali.
Bw. Mabelya ameeleza kuwa katika kuhusiana na katika manispaa ya Temeke wamekuwa wakionyesha juhudi ya kuyatokomeza ukatili licha ya kutokea baadhi ya matukio ambayo kwa sasa wamedhibitiwa.
Inspekta Blandina Ndunguru Kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Polisi Chang’ombe, amesema kuwa ukatili wa watoto umekuwa ukijitokeza katika jamii kutokana na kukosekana kwa elimu, hivyo wamekuwa wakijitahidi kuelimisha umma kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Women Journalist Advocates For Children Right (TAWOJAC) Bi. Magreti Kyando, amesema kuwa wataendelea kufanya kazi na serikali katika kuhakikisha wanatokomeza ukatili dhidi ya watoto.
Bi. Kyando amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni ambazo zilitolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha ukatili unafanyika, hivyo jitiada mbalimbali zinapaswa kufanyika ili kuhakikisha malengo tarajiwa yanafanikiwa.
Hata hivyo wanafunzi kutoka shule mbalimbali wameiomba serikali kudhibiti vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikifanyika katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Kila June 16 yanakwenda sambamba na kauli mbiu ya kitaifa isemayo ‘Tuimarishe Ulinzi wa Mtoto,Tokomeza ukatili dhidi yake,jiandae kuhesabiwa.
Post a Comment