RAIS SAMIA ATATUA CHANGAMOTO YA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA KIJAMII KWA WANAKIJIJI WA LAJA KUPITIA TASAF
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo amempongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa
fedha za ujenzi wa daraja lingine katika Kijiji cha Laja kilichopo Halmashauri
ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za
kijamii katika eneo hilo.
Mhe. Chaurembo ametoa pongezi
hizo baada ya kamati yake kumuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
kuhakikisha TASAF inajenga daraja hilo ili kutatua changamoto iliyokuwa ni
kikwazo kikubwa cha upatikanaji wa huduma za kijamii.
Mhe. Chaurembo amefurahishwa na
kitendo cha Mhe. Mchengerwa kuomba ridhaa ya Mhe. Rais kutoa fedha za TASAF
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya kamati yake yaliyolenga kutatua
changamoto za wananchi wa eneo hilo.
Ameongeza kuwa, kwa kawaida
kamati yake inapofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi, inakuwa
imejiwekea lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo uamuzi wa
Mhe. Rais, umewezesha azma ya kamati yake.
Awali, Mhe. Mchengerwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kutatua
changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo na ndio maana amechukua hatua
madhubuti ya kuwajengea daraja ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za
kijamii.
Amesema pamoja na kukamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha Vijiji vya
Laja na Umbang’w, Mhe. Rais kupitia TASAF ameahidi kujenga daraja lingine katika
korongo lililoko karibu na shule ya Msingi Laja kwani wakati wa masika watoto
wa shule walioko ng’ambo ya korongo wanashindwa kuhudhuria masomo.
“Mhe. Rais ameniagiza niwaambie kwamba, amekubali ombi lenu la kuwajengea
daraja lingine ili wanafunzi waweze kushiriki masomo kikamilifu na wakazi wa
eneo hili washiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” Mhe.
Mchengerwa amesisitiza.
Katika kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais, Mhe. Mchengerwa amewaagiza watendaji
wa TASAF kufanya tathmini ya gharama za ujenzi wa daraja hilo mapema
iwezekananvyo ili ujenzi uanze mapema.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka wananchi wa eneo hilo wakutane kwa ajili
ya kufanya vikao vya tathmini ya miradi ambayo itaingia katika Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Nne ambayo tayari Mhe. Rais ameshatoa fedha kwa
ajili ya utekelezaji wake.
“Viongozi wa kuteuliwa na Viongozi wa kuchaguliwa tujiongeze kwa kuwatumia
wadau wa maendeleo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo
yenu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, kila kiongozi akitumia nafasi yake vizuri
ya kuwahudumia wananchi kwa kutambua dhamana aliyo nayo kuwa ni ya kuwahudumia
wananchi, hakika taifa linaweza kumaliza changamoto kwa wakati.
Akitoa ushuhuda wa namna TASAF ilivyowasaidia kutatua changamoto ya
upatikanaji wa huduma za kijamii katika eneo hilo, mkazi wa Kijiji cha Laja,
Bibi Balbina Sulle ameipongeza TASAF kwa kuwajengea daraja imara ambalo
limerahisisha upatikanaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto na ya elimu kwani
sasa hivi wanafunzi wamekuwa wakishiriki masomo bila kikwazo cha kivuko.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) imehitimisha
ziara yake ya kikazi ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini katika Halmshauri ya Wilaya ya Arusha na Karatu.
Post a Comment