MAAFISA FORODHA MIPAKANI WASISITIZWA JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA SHERIA ZA OSBP ILI KUHAMASISHA WATUMIAJI
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Msafiri Mbibo akiongea na Watumishi wa TRA pamoja na watumishi wengine wa baadhi ya taasisi za Serikali zinazofanya kazi pamoja katika Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Mutukula mkoani Kagera ambapo ni mpakani mwa Tanzania na Uganda, kuhusu namna ya kushirikiana kwa pamoja na kuwa na nidhamu katika kazi zao wanapokua mpakani hapo.
Naibu Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Msafiri Mbibo (wa pili kulia) akiongea na
kutoa maagizo mbalimbali kwaviongozi wa TRA katika ofisi ya TRA iliyopo eneo la
Kyaka mkoani Kagera wakati alipofanya ziara yake ya kikazi mkoani hapo kwa
ajili ya kusikiliza changamoto mbalimbali katika mpaka wa Tanzania na Uganda.
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Msafiri Mbibo akimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustin Kamuzora (kushoto) wakati alipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kufanya nae mazungumzo juu ya masuala mbalimbali ya kodi ikiwemo namna bora ya kuboresha makusanyo ya mapato ya Serikali.
PICHA ZOTE NA TRA
Na. Mwandishi wetu
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), imewataka Maafisa Forodha wa TRA pamoja na maafisa wa taasisi
nyingine za Serikali kuhakikisha kuwa wanahamasisha matumizi sahihi ya kisheria
katika Vituo vya Huduma kwa Pamoja Mpakani ili watu mbalimbali wanaopita
kupitia katika mipaka hiyo waweze kuhamasika kutumia njia sahihi badala ya njia
zisizo rasmi.
Hayo yamesemwa hivi
karibuni na Naibu Kamishna wa TRA, Bw. Msafiri Mbibo wakati alipofanya ziara
yake ya kikazi katika mpaka wa Mutukula unaounganisha nchi ya Tanzania na
Uganda uliopo mkoani Kagera.
Bwana Mbibo amesema
kwamba, lengo la kutaka kuwepo kwa matumizi sahihi ya sheria hizo katika maeneo
ya mipakani ni kuzuia watumiaji kutumia njia zisizo rasmi ambazo zinaweza
kuathiri takwimu za kiuchumi, kuhatarisha usalama wa nchi na pia uingizaji
bidhaa mbazo hazina viwango ambazo zitaumiza walaji wa ndani na zinaweza
kuharibu mahusiano baina ya Tanzania na nchi za jirani.
“Kuziingiza bidhaa
ambazo hazina viwango nchini kwetu na kupeleka bidhaa ambazo hazina viwango kwa
nchi ambazo ni majirani zetu kutaharibu mahusiano yetu ya kibiashara pindi
wakigundua tunaingiza nchini mwao bidhaa za namna hiyo, hivyo lazima tusimamie
vizuri sheria ili mambo haya yasitokee”, alisema Mbibo.
Ameongeza kuwa, mpaka
wa Mutukula kwa sasa ufanisi wake unaoongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa
mwaka wa fedha uliopita wa 2020/2021 ulipangiwa lengo la kukusanya shilingi bilioni
21 na umefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 24 ambapo hiyo ni sawa
ufanisi wa utendaji wa asilimia 114 ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa
2019/2021 malengo yalikua ni kukusanya shilingi bilioni 18 na zikakusanywa
shilingi bilioni 20 na zaidi.
“Mpaka huu ni
wakutegemewa na unafanya vizuri zaidi, na endapo tutazidi kuongeza huduma au
vitendea kazi katika mpaka huu basi ufanisi huu wa sasa utazidi kuongezeka na
tutaweza kuwahudumia wananchi wa nchi jirani na Watanzania pia”
Aidha, amefafanua kuhusu
magari yaliyopo mpakani hapo kwa kusema kwamba, baadhi ya magari ambayo
hayajakamilisha baadhi ya taratibu ndogo ndogo wahusika huwa wanaitwa ili
waweze kukamilisha taratibu hizo ili waweze kulipa kodi zao na kuyaondoa,
lakini pia kwa wale ambao wameyatelekeza magari yao sheria inaitaka TRA
kutangaza kwa muda fulani ili wahusika wenyewe wajitokeze na kukamilisha
taratibu za kiforodha na endapo hawajafanya hivyo baada ya siku kadhaa kupita sheria
inaitaka pia TRA iyaingize magari hayo katika mnada ambao mtu atayevutiwa nayo aweze
kuyanunua ili kodi ya Serikali iweze kukombolewa.
“Mnada wa kuuza magari
yaliyotelekezwa tunafanya kwa njia ya mtandao (Online), hivyo mtu yeyote nchi
nzima anaweza kushiriki katika mnada, lakini kuna baadhi ya magari ya watu
ambao ni wakorofi na wamekua wakichezea chesisi namba za magari na kwa bahati
nzuri sheria inamruhusu Kamishna Mkuu wa TRA kuyatoa kwa namna anavyotaka yeye,
basi sisi tunaweza kuyagawa kwa taasisi nyingine za Serikali lakini hii huwa hatufanyi
mara kwa mara”, alisema Mbibo.
Naibu Kamishna Mkuu wa
TRA yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya ziwa na lengo la ziara
hiyo ni kuona namna ya utendaji kazi wa ofisi za TRA mipakani ikiwemo
kusikiliza changamoto mbalimbali katika ofisi hizo ili ziweze kutafutiwa
ufumbuzi wake na hatimaye makusanyo ya mapato yazidi kuongezeka na kwenda
kuleta maendeleo kwa Taifa.
Post a Comment