Ads

HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM KINARA UKUSANYAJI MAPATO YAKUSANYA SHILINGI BILIONI 40 KINONDONI YA PILI DODOMA YA TATU

 

Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Ummy Mwalimu, akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu  mapato na matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji kwa mwaka wa fedha 2020/21 leo Julai 29,2021 jijini Dodoma.

………………………………………………………………………..

Na Alex Sonna,Dodoma

HALMASHAURI  ya Jiji la Dar es Salaam imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi bilioni 67.09 ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni bilioni 40.7 na Halmashauri ya Jiji la Dodoma bilioni 38.4.

Hayo yameelezwa leo Julai 29,2021 na Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Ummy Mwalimu wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu  mapato na matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Waziri Ummy amesema katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri   ya Jiji la Dar es Salaam imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi bilioni 67.09 ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni bilioni 40.7 na Halmashauri ya Jiji la Dodoma bilioni 38.4.

HALMASHAURI ZAKUSANYA BILIONI 757 SAWA NA ASILIMIA 93

Waziri Ummy amesema kwa mwaka wa fedha 2020/21 Halmashauri zilipanga kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 814.9 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.

Amesema hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2021 Halmashauri zimekusanya jumla ya Shilingi bilioni 757 ambayo ni asilimia 93 ya makisio ya mwaka.

“Mapato halisi kwa mwaka wa fedha yameongezeka kwa Shilingi bilioni 40 sawa na asilimia 6 ikilinganishwa na mapato yaliyokusanywa mwaka wa fedha 2019/20 ambayo yalikua Shilingi bilioni 717 kati ya bajeti ya Shilingi bilioni 765.5,”amesema Waziri Ummy.

HALMASHAURI 57 ZIMEKUSANYA KWA ASILIMIA 100

Amesema ukusanyaji wa mapato ya ndani, unaonesha kuwa Halmashauri 57 zimekusanya kwa asilimia 100 au zaidi ya makisio yake ya mwaka, Halmashauri 90 zimekusanya kati ya asilimia 80 hadi 99 na Halmashauri 37 zimekusanya kati ya asilimia 50 hadi 79.

Amesema ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani unaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale imeongoza katika Halmashauri zote 184 kwa kukusanya asilimia 163 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe asilimia 136 na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro asilimia 133.

Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Mtama asilimia 51, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti asilimia 51 na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli asilimia 52, Halmashauri hizi zimekuwa za mwisho katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Aidha, Halmashauri 10 kati ya 184 zimekusanya kuanzia Shilingi bilioni 10 na zaidi na Halmashauri 9 zimekusanya chini ya Shilingi bilioni 1

KIMKOA NJOMBE KINARA

Aidha,amesema makusanyo Ki-Mikoa, Mkoa wa Njombe umeongoza kwa kukusanya asilimia 113 ikifuatiwa na Mkoa wa Geita asilimia 107,Mkoa wa Songwe asilimia 107 na Mkoa wa Lindi umekua wa mwisho kwa kukusanya asilimia 78 ukifuatiwa na Mkoa wa Simiyu asilimia 81 na Mkoa wa Singida asilimia 82.

JIJI LA MBEYA KINARA MAKISIO

Kwa mwaka wa fedha 2020/21 Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam asilimia 99 na Halmashauri ya Jiji la Mwanza asilimia 92.

Aidha, Halmashauri ya Jiji la Arusha imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya asilimia 80 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma asilimia 82 na Jiji la Tanga asilimia 88.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2020/21 Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 109 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni asilimia 106 na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke asilimia 105.

“Katika kundi hili Halmashauri ya Manispaa ya Lindi imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya asilimia 58 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,”amesema.

Kwa mwaka wa fedha 2020/21 Halmashauri ya Mji wa Njombe imeongoza kwa kukusanya asilimia 131 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Kibaha asilimia 116 na Halmashauri ya Mji wa Mafinga asilimia 108.

Aidha, Halmashauri ya Mji wa Ifakara imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 64 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Miji wa Korogwe asilimia 66 na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba asilimia 70.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2020/21 Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale imeongoza kwa kukusanya asilimia 163 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe asilimia 136 na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro asilimia 133.

Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Mtama na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti zimekuwa za mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 51 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilayaya Bumbuli asilimia 52.

Amesema uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2020/21 unaonesha kuwa matumizi ya fedha za mapato ya ndani katika shughuli za miradi ya maendeleo Halmashauri zimetumia Shilingi bilioni 279.7.

Amesema ni  sawa na asilimia 92 ya fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya maendeleo ambayo ni Shilingi bilioni 303.6 ambazo ni asilimia 40 au 60 ya mapato halisi yasiyolindwa.

“Halmashauri 37 zimetumia asilimia 100 au zaidi ya kiasi kilichopaswa kutumika, Halmashauri 131 zimetumia kati ya asilimia 50 na 99 ya kiasi kilichopaswa kutumika na Halmashauri 16 zimetumia chini ya asilimia 50 ya kiasi kilichopaswa kutumika,”amesema.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa imeongoza kwa kuchangia asilimia 192.3 ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru asilimia 166 na Halmashauri ya Wilaya ya Newala asilimia 155.

Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imekua ya mwisho kwa kuchangia asilimia 25.47 ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe asilimia 28 na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli asilimia 28

Amesema uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2020/21 unaonesha kuwa Halmashauri zimechangia kiasi cha Shilingi bilioni 53.8 kwenda kwenye Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.

“Ikiwa ni asilimia 86 ya kiasi kilichopaswakuchangiwa ambayo ni Shilingi bilioni 62.7 ambayo ni asilimia 10 ya mapato halisi ya vyanzo visivyolindwa kilichokusanywa katika kipindi hicho,”amesema.

HALMASHAURI 120 ZACHANGIA MIKOPO YA WANAWAKE,VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU

Waziri Ummy amesema Halmashauri 40 zimechangia asilimia 100 au zaidi,ambapo  Halmashauri 120 zimechangia kati ya asilimia 50 na 99 na Halmashauri 24 zimechangia chini ya asilimia 50 kwenye Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Chato imeongoza kwa kuchangia asilimia 207 ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu asilimia 183 na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa asilimia 167.

Aidha,Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imekua ya mwisho kwa kuchangia asilimia 13 ifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe asilimia 15 na Halmashauri ya Mji wa Masasi asilimia 21.

CHANGAMOTO

Waziri Ummy amesema katika kufuatilia usimamizi wa mapato ya ndani ya Halmashauri na

matumizi yake,wamebaini changamoto za baadhi ya Halmashauri kutokuingiza taarifa za ukusanyaji mapato kwenye mfumo kwa wakati hivyo, kupelekea ugumu na ucheleweshaji wa uandaaji wa taarifa ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuhusu Mapato na Matumizi.

Ameitaja changamoto nyingine ni baadhi ya Halmashauri kuingiza mapato kwenye vifungu visivyo sahihi hivyo, kupelekea kufanya marekebisho na kuchelewesha uandaaji wa taarifa kutoka kwenye mfumo.

“Baadhi ya Halmashauri kuchelewa kufanya usuluhishi wa taarifa za mapato kwenye mfumo wa Uhasibu hivyo, kuchelewesha uandaaji wa taarifa kutoka kwenye mfumo.Baadhi ya Halmashauri zimeshindwa kufikia malengo ya makusanyo ya mapato ya ndani hivyo, kuathiri utoaji wa huduma kwa jamii ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa miradi ya maendeleo na mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu,”amesema.

UTAUZI WA CHANGAMOTO

Waziri Ummy amesema ili kukabiliana na changamoto hizo Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa zitahakikisha kazi ya uingizaji wa mapato pamoja na usuluhishi wa taarifa za fedha inafanyika kila mwezi ifikapo au kabla ya tarehe 15 baada ya mwezi husika kuisha;

Pia,Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa itaendelea kuzisimamia Halmashauri katika masuala ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya mifumo ili kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato.

“Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea kuboresha mifumo yaukusanyaji wa mapato ya ndani ili kudhibiti mianya ya upotevuwa mapato.Halmashauri zitaendelea kuhimizwa kuchangia miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa mujibu wa Sheria,”amesema.

MAELEKEZO

Waziri Ummy amezitaka Halmashauri ziendelee kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani ambavyo haviitakuwa kero kwa wananchi ili kuongeza uwezo wa utoaji huduma kwa wananchi hususani huduma bora za afya, elimu na miudombinu ya barabara.

Amezitaka Halmashauri ziimarishe usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato ili kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato.

Vilevile,Halmashauri zihakikishe kuwa fedha za makusanyo ya ndani zinazokusanywa zinapelekwa benki ndani ya saa 24 baada ya kuzikusanya.

“Ni marufuku na ni kosa la kisheria kwa Halmashauri kutumia fedha zilizokusanywa kabla ya kuzipeleka benki (fedha mbichi) kwa sababu yoyote ile,”amesema Waziri Ummy.

Aidha,Halmashauri zihakikishe zinapeleka na kutumia angalau asilimia 40 ya mapato yaliyokusanywa (kwa Halmashauri zinazokusanya chini ya Shilingi bilioni 5 kwa mwaka) na asilimia 60 (kwa Halmashauri zinazokusanya zaidi ya Shilingi bilioni 5 kwa mwaka) kwenye miradi ya maendeleo ili kutatua kero za wananchi.

No comments