Ads

ZAIDI YA WAKULIMA 40,000 KUNUFAIKA NA MRADI WA UPIMAJI WA UDONGO NA MAFUNZO YA KILIMO CHENYE TIJA.


Kampuni ya OCP Afrika iliyo kinara katika uzalishaji wa mbolea ulimwenguni, imezindua rasmi awamu ya pili ya mradi wa tathmini ya udongo na kutoa elimu kwa wakulima juu ya afya ya udongo, mbinu sahihi kwa mazao husika.

Uzinduzi wa mradi huu umefanyika Mei 21, 2021 Sumbawanga mjini,   wakulima , wasambazaji, wataalam wa Kilimo na viongozi wa Serikali walishiriki katika uzinduzi wa mradi huo uiofanywa na ndugu Kalolius Misungwi, Mkuu wa wilaya ya Kalambo aliyekua akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ndugu Joseph Mkirikiti.

Kupitia mradi huu wa OCP SCHOOL LAB Wakulima baada ya kupimiwa afya ya udongo watakutanishwa na wataalamu ili kupatiwa mapendekezo sahihi ya matumizi ya mbolea katika mashamba husika.

OCP Afrika kupitia kampuni tanzu ya OCP Tanzania  ilizindua awamu ya kwanza mradi wa tathmini ya udogo mwaka 2019, na awamu hii ya pili ya mradi huo unatarajiwa kuhudumia wakulima na wadau wa kilimo wa mikoa ya Rukwa, Morogoro, Mbeya na Iringa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Idara za Kilimo (taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI) kituo cha Uyole), tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI).

Mradi wa OCP SCHOOL LABUtatoa ushauri sahihi kwa mkulima mmoja mmoja na mapendekezo yanayolenga kuongeza tija ya  mazao kama mahindi, mpunga, viazi pamoja na alizeti.

Mradi huu ni mwendelezo wa awamu ya kwanza iliyozinduliwa mwaka 2019 na kufikia wakulima na wadau wa kilimo 20,000 katika mikoa za Njombe na Songwe. Majibu ya utafiti wa udongo kwenye mikoa hii yameweka bayana kwamba ukiachia mbali upungufu wa madini ya Fosforas na Naitrojeni uliopo kwa kipindi kirefu, kuna upungufu pia wa madini ya Zinki, Salfa pamoja na Potasiamu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Ndugu Joseph Mkirikiti,  Mkuu wa wilaya ya Kalambo Ndugu Kalolius Misugwi alisema, “sekta ya kilimo imeajiri namba asilimia 65% ya watanzania wote na imelihakikishia taifa upatikanaji wa chakula kwa asilimia 100% pamoja na malighafi za viwandani, lakini bado idadi hiyo ya watanzania wanaojishughulisha kilimo haipo katika uwiano sawa na idadi ya watanzania wote nah ii ni kwa sababu ya tija ndogo inayotokana na uzalishaji mazao. Hiyo mpango huu utasaidia kuongeza na tija na bila shaka kuongeza uzaishaji wa mazao ya kilimo”

“Niwapongeze sana kampuni ya OCP Afrika kwa kuandaa mradi huu ili kusaidia kutathimini rutuba ya udongo katika ngazi yamkulima kwa vijiji 400 katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa na Morogoro na kwamba kazi hiyo itafanyika bila malipo yoyote. Aliongeza Ndugu Misungwi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi huo wa mradi wa awamu ya pili mjini Sumbawanga,Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya OCP Tanzania Dkt. Mshindo Msolla alisema, "OCP Tanzania ikishirikiana na Serikali imeandaa mchakato wa upimaji wa udongo kwa zaidi ya vijiji 100 ndani ya mkoa wa Rukwa.

Lengo ni kuwaelimisha wakulima juu ya udongo wa eneo lao bila gharama zozote kwa wakulima hao. Majibu yatatolewa kwao pamoja na ushauri wa kitaalamu juu ya nini kifanyike ili kutunza ubora wa udongo wa kijiji husika kwa matokeo bora ya shughuli za kilimo.

 Katika kila kijiji zaidi ya wakulima 100 watafikiwa na kuelimishwa namna bora za kufanya kilimo kiwe cha mahindi, mpunga au alizeti kulingana na maeneo waliopo. Na kwa mradi huu tunazamia kufikia wakulima 10,000 kwa mkoa wa Rukwa pekee.

Mradi huu wa upimaji na tathmini ya udongo kwa mwaka 2021unatarajiwa kuendeshwa katika vijiji 400 na kuwafikia wakulima wapatao 40,000 kufikia mwisho wa mwaka 2021. Mradi huu pia unatarajiwa kutoa tathmini ya udongo na mapendekezo ya matumizi ya mbolea kwa wakulima wapatao 14,000 watakao wakilisha wakulima wenzao kutoka mashamba mbalimbalikwa kutumia technolojia ya kisasa.



"Ni jambo lenye ulazima, kwamba wakulima wetu wawe rafiki wa teknolojia za kisasa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji wao, na hivyo kuondokana na umasikini. Mradi huu wa upimaji na tathmini ya udongo ni jambo la kipekee sana na hivyo tunahamamisha wakulima wote wawe sehemu ya mradi huu". Aliongeza Dkt. Msolla.

Tangu mwaka 2017 zaidi ya wakulima 390,000 wamenufaika na miradi ya upimaji na tathmini wa udongo kutoka nchi nane barani Afrika za Naijeria, Togo, Ghana, Guinea, Kenya, Burkina Faso, Cote D'Ivoire na Senegal na kwa namna ya kipekee Tanzania inaungana na nchi hizo kuwa moja wa nchi wanufaika wa mradi huo.

Mradi huu wa upimaji na tathmini unaratibiwa kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya kilimo, Tawala za mikoa na Serikali za mitaa pamoja na Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI) wataalamu wa maendeleo ya kilimo.

"Mradi wa upimaji na tathmini wa udongo unaoongozwa na OCP kwa sasa ni nyenzo madhubuti kwa wakulima utakaokua na msaada mkubwa kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji mazao". Alihitimisha Dkt. Msolla.

Kuhusu OCP Afrika:

OCP Afrika ilianzishwa mwaka 2016 ikifanya kazi bega kwa bega na wakulima ili kuleta maendeleo ya Kilimo. Tunazalisha mbolea za aina mbalimbali zinazoendana na uhitaji wa mazao husika, na tunafanya kazi pamoja na washirika mbalimbali zikiwemo serikali za kitaifa, taasisi na mashirika binafsi ili kuwaunganisha wakulima na mahitaji yao, ufahamu na mallighafi ili waweze kufanikiwa.

Tuna uelewa mkubwa juu ya ujitaji wa udongo wa Afrika na tumejiatiti kuipatia Afrika mbolea inayohitajika kwa wakati husika, mahala husika na kwa bei rafiki. Ikiwa na makao makuu yake Morocco, kampuni ya OCP Afrika ni kampuni tanzu ya OCP Group vinara wa uzalishaji wambolea ulimwenguni yenye uzoefu wa miaka zaidi ya 100.  Kwa taarifa zaidi tembelea www.ocpgroup.ma

Kuhusu Taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI)

Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania, taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI) iliundwa ili kutatua changamoto za upimaji udongo, sampuli pamoja na kutoa nasaha zitakazo imarisha ukuaji wa kilimo katika ngazi za vijiji, wilaya na mikoa. Kwa kushirikiana na kampuni ya OCP Afrika na serikali za mitaa.

Kazi kubwa ya mshirika huyu ni kuweka mabaya mapungufu yaliyopo kwenye virutubisho vya udongo na kupendekeza mbolea bora kulingana na mapungufu hayo.

No comments