WAZIRI MKUU AHIMIZA VIONGOZI WA DINI KUHUBIRI AMANI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla watumie nyumba za ibada kuhubiri suala la amani na utulivu.
Akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu alipohudhuria sala ya Ijumaa leo (Julai 17, 2020) katika msikiti wa Buhari uliopo Ruangwa, mkoani Lindi, Waziri Mkuu amesema ni muhimu Watanzania wakajenga tabia ya kuaminiana, kuvumiliana pamoja na kupendana kwani mambo haya yote huchangia uwepo wa amani na utulivu.
“Nchi hii imejizolea sifa kuwa ni nchi ya amani na utulivu kwa sababu jambo hili linahubiriwa na viongozi wa dini zote. Nchi hii sasa imekuwa ni kimbilio la nchi ambazo zimepoteza amani kwenye nchi zao, wanakuja hapa wanajifunza na wakirudi kwao wanaendelea kuwa salama,” amesema.
Waziri Mkuu amesema kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kuzingatia mahubiri ya viongozi wa dini ili nchi iendelee kuwa na amani kwani kukiwa na amani na utulivu lazima maendeleo yataonekana.
“Nchi yetu imekuwa na kasi ya maendeleo katika maeneo mengi. Mimi naamini maendeleo haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na amani tuliyonayo na hii inatokana na mahubiri ya viongozi wetu wa dini. Dini ina mchango mkubwa sana katika uendeshaji wa Serikali,”
Post a Comment