NARCO yamsimamisha kazi Meneja West Kilimanjaro
Na Mwandishi Wetu,
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), Masele Mipawa
amemsimamisha kazi Meneja wa Ranchi ya West Kilimanjaro iliyopo Arusha, Hezron
Kyaruzi kwa tuhuma za kukosa uadilifu kwa mali za Umma na kusababisha upotevu wa
Ng’ombe takriban 32.
Akiwa katika ziara ya kutembelea Ranchi hiyo ya West Kilimanjaro mwishoni mwa wiki
(Julai 18, 2020), Mipawa alisema kuwa waliamua kufanya maamuzi hayo kufuatia
changamoto nyingi zinazoikumba shamba hilo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na
uongozi mbovu wa meneja huyo.
“Kutokana na upotevu wa Ng’ombe, uzembe na ukosefu wa maadili tumeamua
kumsimamisha kazi Meneja wa Ranchi na Msaidizi wake na hatua nyingine za kisheria na
kinidhamu zitafuata,”alisema Mipawa
Mipawa alisema ziara hiyo aliyoifanya katika Ranchi hiyo ni kufanya ukaguzi kutokana na
taarifa walizokuwa wakizipata ambazo zilionesha kuwa katika shamba hilo kumetokea
upotevu wa Ng’ombe ambao Kampuni ya NARCO haina taarifa nao.
“Ziara hii imetusaidia kubaini kuwa kuna wizi uliokithiri katika shamba hili ambao
umechangiwa na mahusiano mabovu kati ya Meneja na jamii inayozunguka shamba hili,
ukosefu wa maadili na uadilifu wa Meneja ambao umepelekea Ng’ombe 32
kupotea,”alisema
“Kati ya ng’ombe hao 32 waliopotea 15 wameshapatikana na wengine 17 hawajapatikana
mpaka sasa huku ng’ombe wengine 27 walichinjwa bila kibali cha makao makuu,”alifafanua
Mipawa
Kufuatia hali hiyo, Mipawa alisema wameamua pia kumsimamisha kazi Msaidizi wake kwa
kuwa alishindwa kumshauri vizuri meneja huyo huku ikidaiwa alikuwa akishirikiana na
meneja huyo kwenda kuazima ng’ombe kwa watu binafsi ili Ranchi hiyo ionekane ina idadi
kubwa ya ng’ombe.
Aidha, Mipawa aliwataka wafanyakazi wengine waliobaki katika shamba hilo kuendelea
kufanya kazi kwa bidii, wazingatie nidhamu na uzalendo huku akiwaonya kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano haitavumilia mtu yeyote anayehujumu rasilimali za Taifa.
Post a Comment