RAIS DKT MAGUFULI AWASHUKURUWATANZANIA KWA KULIOMBEA TAIFA
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza waislam wote nchini kwa kumaliza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na anawashukuru kwa namna walivyoshiriki kuliombea Taifa hasa katika kipindi hiki cha kukabilia na ugonjwa wa COVID-19.
Hayo yamesemwa leo (Jumapili, Mei 24, 2020) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislam mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Eid El Fitri katika Msikiti wa Gaddafi, jijini Dodoma. Pia Rais Dkt. Magufuli amewashukuru waumini wa dini nyingine nchini kwa kushiriki kikamilifu kwenye kuliombea Taifa.
“Leo hii tunamalizia dua ya kumshukru Mwenyezi Mungu, jambo hili Mheshimiwa Rais anasema hatasahau kwa viongozi wote wa dini kuwa pamoja kuliombea Taifa. Pia Mheshimiwa Rais amesema tuendelee na dua zetu, kila mmoja kwa imani yake wakati wote ili Mwenyezi Mungu aendelee kutuondoa katika janga hili ambalo limeleta mtikisiko duniani kote.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania wote kwa ujumla waendelee kushirikiana katika kulifanya Taifa liwe la amani na utulivu. “Dini zetu zinatutaka kila mmoja aendelee kuomba, nchi hii imekuwa na utulivu sana na mfano duniani kwa nchi zinazotaka amani.”
“Tuendelee na tabia hii na vingozi wa dini endeleeni kusisitiza suala la amani, Serikali inawasisitiza muendelee na shughuli zenu, sisi tutahakikisha tunaendelea kulinda amani, fanyeni kazi, mkulima lima na kwa walio viwandani nao waendelee kufanya kazi.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, ambapo amewasisitiza wasiwe na hofu na waendelee kufanya kazi kwa bidii.
Akizungumzia kuhusu hali ya ugonjwa wa COVID-19 ilivyo kwa sasa nchini, Waziri Mkuu amesema katika hospitali ya Amana yupo mgonjwa mmoja, Mloganzila yupo mmoja, Temeke hatuna mgonjwa aliyethibitishwa, Kairuki hakuna mgonjwa, Rabiansia hakuna mgonjwa, Regency hakuna mgonjwa, Aga Khan yuko mgonjwa mmoja, Lulanzi Kibaha wapo wagonjwa 16 na Dodoma Mkonze mpaka leo asubuhi wapo wagonjwa tatu.
Awali, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Mustafa Rajab, amempongeza Rais Dkt Magufuli kwa kuwapa Watanzania moyo wa kishujaa na ujasiri katika kukailiana na ugonjwa wa COVID-19 kwa kuwataka wamwombe Mwenyezi Mungu ili aliepushe Taifa na janga hilo, wakati Mataifa na viongozi wengine duniani yakikumbwa na taharuki.
“Hakuna mkombozi zaidi ya Mwenyezi Mungu, shida zetu, matatizo yetu na hata tukijaribiwa kwa maradhi au mtihani wa aina yoyote Mwenyezi Mungu anatupa ushujaa wa kukabiliana nao. Hofu ya maradhi ni kifo hivyo tusiwe na hofu tumtegemee Mwenyezi Mungu kama Rais wetu anavyotusisitiza.”
Amesema wananchi hawana sababu ya kuwa na hofu kwani tayari Rais Dkt. Magufuli alitangaza siku tatu kwa ajili ya kumuomba Mwenyezi Mungu aliepushe Taifa na corona na viongozi wa dini zote waliitikia wito na waliongoza maombi ambayo yamejibiwa na sasa huo ugonjwa umepungua nchini.
Sheikh Rajab aliongeza kuwa baada ya Mwenyezi Mungu kukubali dua hizo na Rais, Dkt. Magufuli, kutenga siku tatu za kumshukuru Mwenyezi Mungu ambazo zinaisha leo, wananchi hawana budi waendelee kumshukuru na kamwe wasishiriki kwenye kufanya maasi. “Tuwe ni watu wenye kushukuru neema tunazojaaliwa na Mwenyezi Mungu na kamwe tusiwe wenye kuzikufuru.
Post a Comment