Naibu Waziri Ikupa Atoa Msaada Wa Vifaa Kwa Ajili Ya Kukabiliana Na Ugonjwa Wa Corona Kwa Shirikisho La Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata)
Na.Mwandishi Wetu,Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa amekabidhi msaada wa vifaa vya kukabiliana na ugonjwa wa Corona kwa Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kwa ajili ya kusaidia kundi hilo maalum katika kujikinga dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo ikiwemo ndoo za kunawia mikono na mashine maalum ya kunawia pasipo kutumia koki “Free Hand Water Tape” Naibu Waziri, Ikupa alieleza kuwa Serikali inatambua mchango wa Watu wenye Ulemavu na ndio maana viongozi na wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza katika kusaidia kwenye mapambano dhidi ya janga hili la Corona bila kusahau namna ya kuwasaidia watu wenye ulemavu pia katika kuwawekea mazingira wezeshi ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Nikiwa kama mdau nimeona umuhimu wa kukabidhi ndoo za kunawia mikono 90 na mashine maalum ya kunawia pasipo kutumia koki kwa ajili ya kusaidia watu wenye Ulemavu katika mikoa 10 ikiwemo Dar es salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Tanga, Pwani, Iringa na Morogoro,” alisema Ikupa
“Natambua kuwa uhitaji wa vifaa hivyo pamoja na barakoa (Mask), Vitakasa Mikono na Sabuni vinahitajika kwa wingi kwa ajili ya kusaidia watu wenye ulemavu katika maeneo mengine, nitaendelea kuangalia suala la huu uhitaji ili tuendelee kuwezesha kundi hilo maalum zaidi,” alisema
Aliongeza kuwa Serikali imeandaa miongozo katika kipindi hiki inayotazamia namna watu wenye ulemavu wanaweza kusaidiwa wakati huu ambapo mataifa mengi dunia yanaangalia namna bora ya kukabiliana na ugojwa huo, akitolea mfano wa vifaa vya kunawia ambavyo vimeboreshwa na kuwa jumuishi kwa watu wenye ulemavu pia.
Aidha, Naibu Waziri Ikupa alitoa wito kwa kundi hilo maalum kuendelea kufuata maelekezo yanayotolewa na viongozi na wahudumu wa afya Pamoja na kujenga tabia ya kusoma taarifa kwenye mitandao ya kijamii na meseji wanazopata kupitia simu zao za mkononi juu ya kukabiliana na Ugonjwa wa Corona (Covid-19).
Sambamba na hayo Mheshimiwa Ikupa amewataka wadau mbalimbali wenye nia njema kuendelea kujitokeza na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona nchini.
Naye katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Dodoma Bw. Justus Ng`wantalima alitoa shukrani kwa Naibu Waziri na Serikali kwa ujumla kwa kutambua watu wenye ulemavu na kuamua kutoa msaada wa vifaa hivyo ambavyo ni rafiki kwa watu wenye ulemavu na alieleza kuwa vitawafikia walemavu wengi nchini na watanufaika kwa kujikinga na ugonjwa wa Corona.
“Haimanishi kama mtu ni mlemavu basi hawezi kupata maambukizi ya ugonjwa huu wa corona, ugonjwa huo unaweza kumpata mtu yoyote hivyo uwepo wa vifaa hivi utasaidia watu wenye ulemavu kujikinga na janga hilo,” alieleza Ng’wantalima.
Post a Comment