JUNI 30,2020,MKANDARASI ATAKAYESHINDWA KUKAMILISHA REA KUKATWA 10% YA MALIPO YAKE-WAZIRI KALEMANI
Na Zuena Msuya Tanga,
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema mkandarasi yeyote aliyepewa jukumu la kutekeleza mradi ya REA akishindwa kukamilisha kazi hiyo ifikapo Juni 31, 2020 kama ilivyoelekezwa katika makubaliano ya mkataba atakatwa asilimia kumi(10%) ya yalipo yake yaliyosalia.
Dkt. Kalemani alitoa kauli hiyo wakati akifanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa usambazji wa umeme vijijini katika Wilaya za Handeni, Korogwe na Lushoto Mkoani Tanga, Mei 09, 2020.
Alisema kuwa kwa mujibu wa mkataba, wakandarasi wote nchini waliopewa kazi ya kutekeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini wanatakiwa kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Juni 30,2020, kwa wilaya za mikoa yote nchini, na atakayeshindwa kufanya hivyo mradi huo utakabidhiwa kwa mkandarasi mwingine na atakatwa asilimia kumi ( 10%) ya malipo yaliosalia.
Dkt. Kalemani alisisitiza kuwa endapo, mkandarasi atatakwa asilimia kumi (10%) ya malipo yake yaliyosalia,fedha hizo zitapelekwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,( HAZINA) ili zitumike kumlipa mkandarasi mwingine atakayepewa jukumu la kukamilisha mradi huo.
“Hakuna sababu ya msingi ya kumfanya mkandarasi ashindwe kukamilisha mradi huo kwa mujibu mwa mkataba, pia itanishangaza akishindwa kufanya hivyo kwa sababu fedha zote za awali walishalipwa na vifaa vyote vipo na vinapatikana hapa nchini, tunataka kukamilisha kazi hii ndani ya wakati ili tusonge mbele, kwa hili sitamvumilia yeyote”, alisema Dkt. Kalemani.
Katika ziara hiyo Dkt. Kalemani aliwasha umeme katika Kijiji cha Kisasu Kata ya Sindeni wilayani Handeni, pia katika kijiji cha Kwasunga wilayani Korogwe, na katika kijiji cha Kwamsale Kata ya Emtoye wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Aidha aliwaagiza Viongozi wa Serikali za Mitaa waliofika katika shughuli za uwashaji umeme kwa niaba ya wananchi wao,ili kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwa ni tahadhari ya kujikinga na maambuki ya Corona, kuwahimiza na kuwasisitiza wananchi wao kuendelea kulipia gharama za kuunganishwa umeme ya shilingi 27,000 tu .
Pia wasikubali kulipia miundombinu ya umeme kama, nguzo, nyaya, mita za luku na mashineumba kwakuwa tayari zimekwisha lipiwa na serikali.
Katika ziara hiyo pia alitembelea Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Kilole kilichopo wilayani Korogwe mkoani Tanga, kilichojengwa mwaka 1929 chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2.5 ambacho kwa sasa kinafanyiwa ukarabati mkubwa.
Dkt. Kalemani aliuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Nchini( TANESCO) kukamilisha ukarabati huo ifikapo June 15, 2020, mwaka huu ili kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme kwa wakazi wa Walaya ya Korogwe mkoani humo.
Vilevile aliuagiza TANESCO kutafuta eneo kubwa zaidi ili kukihamisha kituo hicho ambacho kiko katika eneo finyu na kimezingirwa na makazi ya watu.
Alisema kuwa endapo kituo hicho kitahamishiwa katika eneo kubwa zaidi kitakuwa na fursa ya kuongezewa uwezo zaidi na hata kujengwa mitambo mingine mikubwa ya kupoza na kusambaza umeme kwa watumizi mengine hapo baadaye.
Ukarabati unaofanyika katika kituo hicho ni kufunga mashineumba mpya yenye uwezo wa kuzalisha Megawati tano za umeme, kuweka vifaa na miundombinu mipya ya kituo hicho pamoja na kutenganisha njia za kusafirisha umeme kutoka katika kituo hicho kwenda kwa watumiaji.
“Mnasubiri nini kufunga hii mashineumba ambayo imefika hapa miezi miwili iliyopita?,pia harakisheni ukarabati kwa kubadilisha miundombinu ya kituo hichi, iliyopo hapa ni chakavu si mnaiona na niyazamani sana jamani,wananchi watanga wanataka umeme mwingi na wa uhakika, na marufuku kukatika umeme kwa mkoa huu mara baada ya kukamilika kazi hii”, alisisitiza Dkt. Kalemani.
Kuhusu suala la wizi wa umeme na miundombinu yake, Dkt. Kalemani alisema kuwa yeyote atayebainika kufanya vitendo vya wizi ni muhujumu uchumi hivyo achukuliwe hatua za kisheria.
Aliwataka wananchi kwa kushirikiana na mamlaka husika kulinda miundombinu ya umeme pia kuwaweka bayana na kuwataja wale wote wenye tabia ya wizi ili wachukuliwe hatua, kuepuka kuleta usumbufu kwa wananchi kwa kukosa huduma ya umeme na hasara kwa serikali.
Post a Comment