Ads

TGNP YATOA TAMKO KUHUSU VIRUSI VYA CORONA


Mkurugenzi Mtendaji wa  Jinsia Tanzania TGNP Lilian Liundi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

VIRUSI VYA KORONA NA ATHARI ZAKE KWA WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE
Mnamo Machi 16 2020, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu alithibitisha kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza nchini wa ugonjwa unaosababibwa na virusi vya Corona, maarufu kama COVID-19.


Kutokana na tatizo hilo ambalo limetangazwa na Umoja wa mataifa kuwa Janga la dunia, Serikali  imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huu ikiwemo kufunga shule na vyuo, kutoa elimu na kuhamasisha jamii kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwa kuepuka kukaa kwenye misongamano ya watu, kunawa mikono mara kwa mara, na pia, kuanzisha namba maalumu za kupiga ili kutoa taarifa za watu wanaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo au kupata taarifa sahihi juu ya ugonjwa huu wa COVID-19.  Wizara pia imejengea uwezo wanajamii waelemishaji wa majumbani ili kurahisisha ufikishwaji wa taarifa na elimu kwa makundi ya  kijamii. 

Ikumbukwe kuwa yatokeapo majanga kama haya, wanawake  na watoto ndio waathirika wakubwa. Hata janga hili la COVID-19 limeleta changamoto kubwa sana kwa wanawake. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Ajira Duniani (ILO) 2006, zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wapo katika ajira zisizo  rasmi kama vile masokoni ambapo kuna mikusanyiko mikubwa sana jambo ambalo linawaweka katika hatari kubwa sana ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Tukitambua kwamba takribani asilimia 24.5 (2016) ya kaya nchini zinaendeshwa na wanawake na hivyo kuwapa jukumu la kutafuta riziki na kuhudumia familia hii pia inawaweka kwenye hali hatarishi. 

Aidha kundi hili pia kwa miaka mingi limekuwa ni kundi ambalo lipo chini kielimu. Taarifa ya UNESCO ya 2019, kiwango cha elimu kwa watu wazima ni 77.89%. Ambapo wanaume ni 83.2%, na wanawake ni 73.09%. Takwimu hizi ni ushahidi wa wazi kuwa wanawake wameachwa nyuma katika masuala mbalimbali. Tofauti hiyo ya wanawake kuwa nyuma utaiona pia katika nyanja ya ufikiwaji wa taaarifa sahihi kwa wakati mfano magazeti, radio, televisheni na  namitandao ya kijamii. Hali hii kwa kiasi kikubwa inatokana na mifumo wa jamii zetu ya kutokuwa na mgawanyo sawa wa majukumu.

Wanawake kwa kiasi kikubwa wameelemewa na majukumu ya kulea familia na kazi za kutoa huduma  ambazo zinapelekea kukosa muda kabisa  wa majukumu ya kiuchumi, kisiasa, na hata kupata taarifa sahihi na kwa wakati. Kwa kipindi hiki cha janga laCOVID-19, upatikanaji wa taarifa sahihi ni haki kwa kila mwananchi. Hivyo ni muhimu mbinu zinazotumika ziangalie mahitaji ya taarifa kwa makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na vyombo na muda sahihi wa kupeleka taarifa kwa makundi hayo.

Janga hili la  virusi vya corona limeibua changamoto mpya katika familia na jamii zetu hususani kwa watoto wa kike na hata wa kiume ambao shule zimefungwa na wapo majumbani. Watoto wa kike wapo katika hatari ya kupata mimba za utotoni na aina nyingine za ukatili wa kijinsia  kwa sababu watoto ( wakike na wakiume)  wakiwa nyumbani, wazazi wanakuwa kazini. Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 60 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hutokeamajumbani na wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu au majirani.

Kwa ujumla, ukatili wa kijinsia huongezeka sana wakati wa majanga kama haya, si tu kwa watoto bali pia kwa wanawake. Taarifa kutoka nchi za China, Ulaya na Marekani zinaonesha kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia toka COVID-19 ilipoanza. Kwa mfanotaarifa za polisi  nchini China zinaonesha kuwa  ukatili wa kijinsia umeongezeka mara tatu katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 ndani ya mwezi Februari pekee .

Taarifa ya shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema kuwa katika janga hili la Corona wanawake wapo hatarini sana kufanyiwa ukatili wa jinsia kutokana na msongo wa mawazo, kuongezeka kwa majukumu ya nyumbani hasa kipindi hiki watoto wapo nyumbani  na pia, kuweko kwa uwezekano wa ukatili wa wanandoa kuongezea kutokana na msisitizo wa watu kukaa nyumbani ikiwa hawana shughuli za msingi sana zitakazowalazimisha kutoka ndani.

Vile vile, ikumbukwe kuwa wanawake wengi wapo katika sekta isiyo rasmi, wakijishughulisha na shughuli mbalimbali kama vile mama ntilie, biashara masokoni, shughuli ndogo ndogo za viwandani na wafanyakazi wa majumbani, kazi ambazo zinahusisha kutoka mazingira ya nyumbani na kukutana na watu, mara nying katika mazingira yenye misongamano. Hali hii inawaweka katika mazingira hatarishi ya kupata virusi hivi vya Corona -COVID 19. Ni muhimu sana kuweka mikakati madhubuti ya kuwalinda kwa kuwafikia na kuwapelekea huduma na elimu huko waliko ili waweze kujikinga.

Kwa upande wa Afya ya Uzazi ya mama na mtoto, ukweli wakitabibu kuhusu mwanamke mwenye ujauzito na aliyetoka kujifungua ni kuwa, kinga zake si imara sana hususan  kwa kipindi anaponyonyesha. Kwa hospitali zilizo na wauguzi wanawake wazazi wa chini ya mwaka mmoja, tunashauri kuwa wasipangiwe majukumu ya kuhudumia wagonjwa wa Corona. Hii ni vivyo vivyo kwa wanawake wajawazito pia, ambapo siyo wale tu walio kwenye sekta ya afya, bali hata wale walio kwenye jamii zetu. Ni vema wao wenyewe kujilinda, jamii, waajiri, serikali tuwalinde kwa kuwaepusha na misongamano.

Aidha, katika huduma za kliniki kwa wajawazito na watoto, ambapo mara nyingi huwa na msongamao wa watu, ni vyema kusisitiza kuhusu taratibu za kujikinga ikiwemo kunawa mikono, kupata huduma wachache wachache  kwa kukaa mbali kwa mita moja toka mtu na mtu, huku wakijipanga kwa foleni.

Tunatambua kuwa Janga hili limechukua umakini mkubwa sana wa watoa huduma wa afya katika kuhakikisha kuwa ugonjwa unazuilika na kuwatibu wale wanaokuta na ugonjwa na hata serikali kutenga hospitali maalumu za kuwahudumia wagonjwa wa Corona, ni muhimu pia kuhakikisha mizani ya utoaji huduma hospitalini imekaa sawa kwa kuhakikisha pia huduma za kina mama wajawazito na watoto zinaendelea kupewa kipaumbele ili kuendelea kupunguza vifo vya kina mama na watoto vitokanavyo na uzazi.

Ni muhimu sana wazazi wote, baba na mama kuhakikisha kuwa wanawajibika kujikinga wanapokuwa katika shughuli zao zinazowalazimu kutokaa nyumbani kwa sasbabu ikitokea mzazi ameambukizwa akirudi nyumbani ataweza kuwaambukiza watoto, na hivyo juhudi ya sekikali kuwalinda watoto haitokuwa na maana. Hii ndiyo maana ni muhimu kujilinda wewe kwanza, na kufanya hivyo utawalinda mke, watoto na wazee wetu ambao wapo nyumbani muda mrefu kuliko wanaume.

Pamoja na utaratibu mzuri wa watu kutosimama kwenye vyombo vya usafiri, hasa maeneo ya mijini, bado uhaba wa usafiri unapelekea watu wanagombania kuwahi nafasi za kuketi kwenye mabasi, jambo ambalo  ni hatarishi kwa maambukizi kwa watu wengi wanaotumia usafiri wa uma. 

Jitihada zimeanza kuonekana kwa baadhi ya safari kuwa na utaratibu wa kupanda kwa mstari, lakini bado tunaomba utaratibu huu uwe endelevu na ikiwezekana kuwe na tamko toka serikalini. Hii itasaidia kutokuambukizana lakini pia itapandisha hadhi ya usafiri wa umma na kuufanya salama kwa makundi yote ndani ya jamii kama wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu ambao kimsingi kugombania usafiri kumekuwa ni changamoto kwao. Utaratibu huu wa kupanga mstari ufanyike kwenye huduma zingine zote hata katika manunuzi ya bidhaa mbalimbali.

Kuna huduma pendwa na wanawake lakini wakati huu wa janga la Corona hatuna budi kuongeza umakini. Huduma hii kwa wakati mwingine haina tofauti na ya watoa huduma mahospitali, hivyo basi, swala la kuzingatia unawaji wa mikono, kutokugusana na kuzuia urukaji wa mate ni lazima uzingatiwe. Wamiliki na watoa huduma wa saluni za kike na za kiume na hata wanaosafisha kucha, tujilinde kwa kuzingatia taratibu zilizotolewa na Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani.
Watoto wapo majumbani kufuatia shule na vyuo kufungwa, Watoto wanawajibu wa kujifunza na kusaidia kazi za nyumbani. Pamoja na ukweli huo, ni angalizo letu kwa wazazi kuwa watoto hasa watoto wa kike hawa wanapaswa kusoma ili waendelee vizuri watakapo rejea shuleni. Mgawanyo wa majukumu ni vema kuzingatiwa lakini pia haki za watoto pia.

No comments