Ads

TATIZO LA UPATIKANAJI WA BARAKOA KUWA HISTORIA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali imejipanga kuzalisha zaidi ya Barakoa Milioni tatu na nusu kwa mwezi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote hususani katika kipindi hichi cha Janga la Corona.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokua katika ziara ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa (face mask) na Vitakasa mikono (Hand sanitizer) ambapo amefanya ziara hiyo imefanyika katika Kiwanda cha Uzalishaji cha Prestine, Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars na Kiwanda cha Uzalishaji Mafuta na Vilainishi cha Total.

Hata hivyo,Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uzalishaji wa Barakoa za kutosha kwa sasa ni muhimu sana na Serikali itjhakikisha  Viwanda hivyo vinapata malighafi ya kutosha ili viendelee kuzalisha vizuri.

“Kiwanda cha Prestine sasa hivi kinatengeneza Barakoa elfu thelathini kwa siku (30,000) lakini baada ya vifaa kuingia kitazalisha elfu hamsini kwa siku (50,000) na Kiwanda cha Five Star kitazalisha barakoa laki moja kwa siku (100,000) hivyo kwa ujumla Viwanda hivi vitazalisha barakoa zisizopungua milioni tatu na nusu kwa mwezi mmoja (3,500,000) hii ni hatua muhimu sana.”amesema Waziri Bashungwa.

Akizungumza kuhusiana na ziara yake katika Kiwanda cha Total Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uongozi umekubali kushirikiana na Serikali katika kuzalisha vitakasa mikono na tayari maandalizi ya awali yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuangalia sehemu ambayo itatumika kwa ajili ya uzalishaji.

“Baada ya kuangalia Kiwanda na eneo maalumu ambalo wamelitenga kwa ajili ya uzalishaji wa vitakasa mikono, na kwa uwezo wa kiwanda hiki kwa siku kitakua na uwezo wa kutengeneza lita elfu sita (6000) ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kudhibiti ugonjwa huu.” Aliongeza Waziri Bashungwa.

Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuzingatia melekezo na kanuni za kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona (COVID -19).

No comments