DKT.GWAJIMA AMEZITAKA KAMATI ZA AFYA ZA MSINGI HALMASHAURI NA MIKOA (PHC) KUANDAA MIKAKATI MADHUBUTI YA KUPAMBANA NA TISHIO LA UGONJWA WA COVID-19 (CORONA)

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima akinawa mikono katika moja ya sehemu iliyotengwa na uongozi wa Hospitali ya Mvumi leo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Chamwino mkoani Dodoma kwa lengo la kuangalia uelewa wa wananchi kwenye kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID-19(CORONA).
Na. Majid Abdulkarim.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka Kamati za Afya za Msingi za Halmashauri na Mikoa (PHC) kuandaa mikakati madhubuti ya kupambana na tishio la ugonjwa wa COVID-19 (CORONA).
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka Kamati za Afya za Msingi za Halmashauri na Mikoa (PHC) kuandaa mikakati madhubuti ya kupambana na tishio la ugonjwa wa COVID-19 (CORONA).
Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Chamwino mkoani Dodoma kwa lengo la kuangalia uelewa wa wananchi kwenye kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa huo.
Akizungumza Dkt. Gwajima amesema Kamati za Afya za Msingi za Halmashauri na Mikoa (PHC) zote nchini wahakikishe wanao mpango kazi wa namna watakavyo wezesha uhamasishaji wa jamii juu ya mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo .
”Kuna haja ya kila chombo kwenye mamlaka zote kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa jamii anayoiongoza na kuhudumia ili jamii na mtu mmoja mmoja waweze kuchukua tahadhari ya ugonjwa huu na kuzuia usiingie nchini” ameelekeza Dkt Gwajima.
Pia Dkt. Gwajima amesisitiza taasisi zote, sehemu za huduma za jamii na kila kaya kuweka sehemu za kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ikiwa ni sehemu moja wapo ya tahadhari muhimu sana sambamba na kuachana na tabia ya kusalimiana kwa kushikana mikono.
“Ili kufanyikisha kuhamasisha jamii kupata uelewa juu ya ugonjwa huu ni vyema kila kiongozi kutekeleza majukumu yake kwa kutumia takwimu kutathmini ufanisi wa kila mkakati ili kuweza kufikia mafanikio makubwa juu ya uchukuaji wa tahadhari juu ya ugonjwa huu”, amesema Dkt. Gwajima.
Vilevile, Dkt. Gwajima amesisitiza Viongozi kuwafikia wananchi na kutathmini jinsi gani wanatekeleza maelekezo yanayotolewa na wataalamu.
Awali katika ziara yake Dkt. Gwajima amekagua ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Uhuru inayojengwa katika halmashauri ya Chamwino na kumtaka msimamizi wa ujenzi huo Gabriel Mkuele kukamilisha ujenzio kwa wakati japo kuwa kulikuwa na changamoto ya hali ya hewa.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Best Magoma amesema kuwa tayari kila kituo katika kila halmashauri kimeshatenga sehemu maalumu ya kuwaweka watu watakao bainika kuhitaji uchunguzi zaidi iwapo wana maambukizi ya virusi vya COVID-19(CORONA) na pia sehemu za kupatiwa matibabu zaidi zimeshatengwa.
Katika ziara hiyo wananchi waliyokuwa wakipatiwa huduma katika hospitali ya Mvumi wamemuomba Dkt.Gwajima na watendaji wake kuhakikisha wanaendelea kuwajengea wananchi wote uelewa juu ya ugonjwa wa COVID-19(CORONA) ili kila kaya ifahamu vema.
Hayo ni maoni ya wananchi baada ya Dkt. Gwajima kutaka kufahamu ni kiasi gani jamii inauelewa juu ya Ugonjwa huo.
Aidha, Dkt Gwajima amewapongeza wadau wote kwa jinsi wanavyotekeleza kwa kasi kubwa usiku na mchana mikakati endelevu ya kuhakikisha tishio la ugonjwa huu linadhibitiwa.
Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa COVID-19 (CORONA) ulianzia katika taifa la China na mpaka sasa umeenea baadhi ya mataifa japo kwa Tanzania bado haujafika hivyo, kila mtanzania ni wajibu wake kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi kama wataalamu wanavyo elekeza.
Post a Comment