ATCL YASITISHA SAFARI ZA NJE YA TANZANIA KUANZIA MACHI 25,2020

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), inasikitika kuwataarifu wateja wake wote na wananchi kwa ujumla kwamba inasitisha safari zake za nje ya Tanzania kuanzia 25 Machi, 2020 hadi hapo tutakapotoa taarifa nyingine ya kurudisha safari hizo hali itakaporuhusu. Safari zilizoathirika ni pamoja na Entebbe (Uganda), Bujumbura (Burundi), Hahaya (Comoro), Lusaka (Zambia) pamoja na Harare (Zimbabwe). Kusitishwa kwa safari hizi kunatokana na mwendelezo wa matamko na maagizo yanayotolewa na serikali mbali mbali katika nchi tunazofanya safari zetu. Matamko hayo ni ya kufunga mipaka na kupunguza mwingiliano kwa sababu ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya aina ya Corona. (COVID-19)
ATCL itaendelea kutoa huduma katika safari za ndani japo kwa kupunguza miruko katika baadhi ya vituo kutokana na upungufu wa abiria wanaosafiri na hasa kipindi hiki ambacho tahadhari nyingi zinatolewa kwa umma kuachana na safari zisizo za lazima.
ATCL inapenda kuwahahikishia wateja wetu kuwa inajali usalama wa vyombo, pia usalama na afya za wafanyakazi, abiria na wateja wetu kwa ujumla. Hivyo tunahakikisha wafanyakazi wanajikinga (kwa kuvaa glovu na barakoa wawapo kazini na ndani ya ndege), tunapulizia dawa na kusafisha maeneo yote ndani ya ndege zetu kwa dawa maalumu, pia tumeweka madawa maalumu ya kusafisha mikono ofisini, airport kabla ya kupanda ndege na ndani ya ndege.
Abiria wote wenye tiketi za ATCL katika safari zilizositishwa wanashauriwa kuwasiliana na ofisi za ATCL au mawakala wa safari za Ndege kwa taratibu za kubadilisha tiketi ili zitumike baadae katika safari zao bila makato yoyote. Tunawaomba radhi wateja wetu wote kwa usumbufu utakaojitokeza kutokana na kusitishwa kwa safari hizo. Kwa taarifa na ufafanuzi zaidi usisite kuwasiliana nasi kupitia na 0800 110 045.
Post a Comment